Mei 3,2022; Jumanne: Juma la 3 la Pasaka

Wat. Filipo na Yakobo.
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO I: 1Kor. 15:1-8

Ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 19:1-4

 1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
  Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
  Mchana husemezana na mchana,
  Usiku hutolea usiku maarifa.

(K) Sauti yao imeenea duniani mwote.

 1. Hakuna lugha wala maneno,
  Sauti yao haisikilikani.
  Sauti yao imeenea duniani mwote,
  Na maneno yao hata miishi ya ulimwengu.
  Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)

INJILI: Yn. 14:6-14
Yesu alimwambia Tomasi: “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.” Filipo akamwambia, “Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.” Yesu akamwambia, “Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, ‘Utuonyeshe Baba?’ Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.”

TAFAKARI
YESU NJIA UKWELI NA UZIMA : Mitume Filipo na Yakobo waliipokea, wakaiishi na kuihubiri injili ya Kristo. Fumbo la imani yetu linatuonyesha Kristo aliyekufa, aliyefufuka na atakayekuja tena. Alionyesha njia iendayo kwa Baba, akahubiri ukweli unaomwokoa mwanadamu na akamletea uzima usiokuwa na mwisho. Yesu ni njia ya kweli iendayo katika uzima. Filipo alitamani Yesu amwonyeshe Mungu amjue. Lakini Kristo anamfumbua macho kwamba, aliyemwona yeye amemuona Baba. Maana Yesu na Baba ni mmoja. Pia yote aliyoyatenda Yesu, aliyatenda kwa amri ya Baba. Yakobo alifundisha na kuandika kuhusu hii njia ya kweli iendayo katika uzima.
Tujaliwe kuwa wafuasi wa Kristo kama watakatifu Filipo na Yakobo. Tumtambue kama sura halisi ya Mungu Baba, na tumtumainie ili atufikishe katika uzima usioisha.

SALA: Ee Mungu, Mwanao amejidhihirisha kwetu kama njia, ukweli na uzima. Tunakuomba utujalie kumfuata kwa uaminifu, ili tuijue kweli itakayotujalia uzima usioisha.