Aprili 30, 2022; Jumamosi: Juma la 2 la Pasaka

Pio V, Baba Mtakatifu
Nyeupe

SOMO 1: Mdo. 6:1-7

Siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’niko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, “Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.” Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa Imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile imani.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 33:1-2, 4-5, 18-19

 1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
  Kusifu kunawapasha wanyofu wa moyo.
  Mwimbieni wimbo mpya,
  Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.

(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tulivyokungoja Wewe.

 1. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
  Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
  Huzipenda haki na hukumu,
  Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
 2. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao
  Wazingojeao fadhili zake.
  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
  Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

INJILI: Yn. 6:16-21

Jioni wanafunzi walitelemka baharini; wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, “Ni mimi, msiogope.” Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.

TAFAKARI
NI MIMI MSIOGOPE: Juzi, Yesu alilisha watu zaidi ya elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili. Leo pia anafanya muujiza mwingine wa kushinda nguvu za uoepo na maji. Wanafunzi wanapanda chomboni kuvuka Bahari ya Kapernaumu. Bahari inachafuka na upepo unavuma. Kwa vile kulikuwa giza, uwoga unawaingia. Wangali katika woga huo, wanamwona Yesu anakwenda juu ya bahari. Wanaogopa kwa sababu, kulingana na simulizi nyinginezo, baharini kuna mambo na viumbe vya kutisha. Pia wanashangaa kitu kinatembea juu ya maji. Kwa vyovyote walidhani watadhuriwa. Lakini Kristo anajitambulisha. Anakaribia chombo, hali inakuwa shwari. Wanaifikia nchi walikokuwa wakienda. Katika maisha tuna changamoto nyingi zinazotuogopesha. Tuna kosa matumaini, tunakata tamaa. Tunaona giza mbele yetu. Kristo daima anatuambia “ni mimi msiogope!” Pengine kuna lile ambalo linakukatisha tamaa kabisa na kukukosesha matumaini, hatuna haja ya kuhangaika, tumwangalie Kristo ambaye daima anatuambia ni mimi msiogope. Mwemnyezi Mungu anatusikia. Tumkimbilie yeye!

SALA: Mwenyezi Bwana wetu, tunakukimbilia tukikuomba utuepushe na kitisho cha ugonjwa wa Korona unaotukosesha matumaini. Amina.