Aprili 28,2022; Alhamisi: Juma la 2 la Pasaka

Mt. Petro Shanel, Padre na Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mdo. 5:27-33

Walipowaleta mitume, waliwaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, “Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.” Petro na mitume wakajibu, wakisema, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.” Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 34:1, 8, 15-19

 1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
  Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
  Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
  Heri mtu Yule anayemtumaini.

K “Maskini aliita, Bwana akasikia.”

 1. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
  Na masikio yake hukielekea kilio chao.
  Walilia, naye Bwana akasikia,
  Akawaponya na taabu zao zote. (K)
 2. Bwana yu karibu nao waliovunjiaka moyo,
  Na waliopondeka roho huwaokoa.
  Mateso ya mwenye haki ni mengi,
  Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)

INJILI: Yn. 3:31-36

Yohane Mbatizaji aliwaambia wafuasi wake, “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote. Yale aliyoyaona na kuyasikia ndiyo anayoyashuhudia, wala hakuna anayekubali ushuhuda wake. Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli. Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo. Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake. Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.”

TAFAKARI
USHAHIDI WA YOHANE MBATIZAJI: Yohane Mbatizaji ndiye nabii wa mwisho kabisa aliyeshuhudia kumalizika kwa Agano la Kale na kufungua Agano Jipya. Yeye alimalizia zama za kinabii na akamwandalia njia Bwana wetu Yesu Kristo. Wengi waliouona utumishi wake, walidhani kwamba pengine yeye ndiye Masiha. Lakini yeye hakujikweza, ila aliweka bayana kuwa yeye siye Masihi. Katika Injili ya leo tunamuona Yohane mbatizaji akitoa ushuhuda wa huyo ambaye anakuja. Anasema huyo anayekuja anatoka juu. Yeye atakapokuja atayanena mambo ya huko juu. Yohane Mbatizaji anashuhudia kazi ambazo Kristo atakuja kuzifanya. Zaidi, anasema yeye atanena maneno ya Mungu kwa sababu atakuwa na Roho wa Mungu Baba. Baba anampenda Mwana na amemjalia vyote. Mwisho anawahimiza watu wamwamini huyo Mwana kusudi wawe na uzima. Aasiomwamini, adhabu ya Mungu itawakalia. Tuna sababu gani tena ya kutafuta ushahidi mwingine. Na tuuige mfano wake, tusijikweze na hapa kupoteza nafasi ya kumtambulisha Kristo kwa watu. Hatima ni wote wamfahamu Kristo aliye Mkombozi wao.

SALA: Ee Mungu Baba yetu, utusaidie pale ambapo tunaenda kumuhubiri Yesu Kristo, ili watu wamwamini na waokoke.