Aprili 27,2022; Jumatano: Juma la 2 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mdo. 5:17-26

Aliondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza. Lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, “Enendeni mkasimame hekaluni, mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu”. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, “Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani.” Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, “Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.” Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 34:1-8

 1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
  Sifa zake si kinywani mwangu daima.
  Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
  Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

K “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.”

 1. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
  Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
  Nalimtafuta Bwana akanijibu,
  Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
 2. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
  Wala nyuso zao hazitaona haya.
  Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
  Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
 3. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
  Akiwazungukia wamchao na kuwakoa.
  Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
  Heri mtu yule anayemtumaini. (K)

INJILI: Yn. 3:16-21

Yesu alimwambia Nikodemo, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.”

TAFAKARI
MUNGU ALIUPENDA ULIMWENGU: Wapendwa, katika injili tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo akiendelea kuongea na Nikodemo. Lakini leo anamuelezea upendo mkubwa wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Upendo ambao Mwenyezi Mungu aliamua kumtoa mwanawe wa pekee kuja ulimwenguni kutuokoa. Huyo mwanawe lengo likiwa kwamba, amwage damu yake kwa ajili ya kukomboa ulimwengu. Damu yake imekuwa fidia ya dhambi alizotenda mwanadamu kupitia kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Hawa. Na hivyo sasa anakuja kulipia uharibifu huu ili kwamba sisi, tuwe na stahiki ya kurudi tena kwa Mungu. Tunapaswa kumuamini, na anayemuamini yeye ataokolewa katika yeye. Lakini asiyemwamini atahukumiwa, kwa sababu hakumwamini mwana wa pekee, aliyekuja kama nuru ulimwenguni. Ni ajabu kuwa twapenda giza badala ya nuru. Kupenda giza ni kutenda matendo maovu. Watenda maovu hutenda wakidhani hakuna anayewaona. Ila Mungu anaona yote. Wapendwa lazima tuthamini upendo huu wa Mwenyezi Mungu kwetu. Nasi tutafaidi na kuuonja upendo huo. Mateso na kifo cha Bwana wetuYesu Kristo pamoja na ufufuko wake, vitakuwa bure kama hatutafaidiki.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi nakuomba unijalie uchaji wako, nimtii mwanao na kumfuata kiaminifu na hatimaye nifaidi wokovu anaotupatia. Amina