Aprili 26,2022;Jumanne: Juma la 2 la Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mdo. 4:32-37

Jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.

Wimbo Wa Katkati: Zab. 93:1-2, 5

 1. Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
  Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.

K: Bwana ametamalakai, amejivika adhama.

 1. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
  Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
  Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)
 2. Shuhuda zako ni amini sana;
  Utakatifu ndio uifaao nyumba yako.
  Ee Bwana, milele na milele. (K)

INJILI: Yn. 3:7-15

Yesu alimwambia Nikodemo, “Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.” Nikodemo akajibu, akamwambia, “Yawezaje kuwa mambo haya?” Yesu akajibu, akamwambia, “Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu. Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.”

TAFAKARI
KRISTO, MFANO WA NYOKA JANGWANI: Leo Kristo anaongea na Nikodemo. Huyu alikuwa mfuasi wake ambaye alikuwa anapenda kumsikiliza na kufundishwa naye. Alifanya hivyo kwa siri kwa sababu aliwaogopa Wayahudi kwa maana yeye alikuwa mmoja kati ya viongozi wakubwa wa dini ya Kiyahudi. Kwa kumsikiliza Kristo, Nikodemo anafaidika na ukweli kwamba Kristo angali hapa duniani watu watapata shida kumuamini. Lakini atakapoinuliwa kila mtu atamwamini naye atakuwa na uzima katika yeye. Kristo anatolea mfano wa yule nyoka wa shaba kule jangwani. Wana wa Israeli walipomkosea Mungu, aliwatumia nyoka wa sumu, waliowaua wengi. Baada ya Musa kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu, Mungu akamwambia Musa akatengeneza nyoka wa shaba. Watu waliomtazama yule nyoka baada ya kuumwa na nyoka wa sumu, walipona. Kilichowaponyesha hawa watu ni kulainisha mioyo yao na kukubali kumtazama yule nyoka. Pengine, kuna wengine ambao waliendeleza ujeuri wao. Hao walikufa. Nasi tukiendelea na ujeuri wetu, tukiendelea na kiburi chetu na ujuaji hatutaweza kuokoka. Lakini tutakapolainisha mioyo na kumwangalia Kristo hakika wokovu utakuwa pamoja nasi.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu lainisha mioyo yetu, tumwangalie Kristo kwa Imani tuweze kupata kuokoka.

AAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAA