Aprili 25,2022 Jumatatu: Juma la 2 la Pasaka

Mt.Marko, Mwinjili.
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO I: 1Pet. 5:5-14

Ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza u na yeye hata milele na milele. Amina. Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo. Mwenzenu mteule hapa Babeli awasalimu, na Marko mwanangu. Salimianeni kwa busu la upendo. Amani na iwe kwenu nyote, mlio katika Kristo. Amina.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 89:1-2, 5-6, 15-16

 1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
  Kwa kinywa change nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
  Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
  Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.

K: “Fadhili zako nitaziimba milele, Ee Bwana.”

 1. Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako,
  Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
  Maani ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana?
  Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa alaika? (K)
 2. Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,
  Ee Bwana, huenenda katika nuru ya uso wako.
  Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,
  Na kwa haki yako hutukuzwa. (K)

INJILI: Mk. 16:15-20

Yesu aliwaambia wale Kumi na mmoja, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.” Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao, akachukuliwa juu mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Nao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, na kulithibitisha lile neno kwa ishara zilizofuatana nalo.

TAFAKARI
AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA: Jana Kristo alitoa ujumbe kwa mitume wake na wafuasi wake kwenda kuihubiri injili kwa kila kiumbe. Leo anaendelea kusema kwamba atakaye amini na kubatizwa ataokoka, lakini asiye amini atahukumiwa. Maana yake ni kwamba Kristo hakuweza kuzunguka ulimwenguni kote kueneza Habari Njema ya wokovu wa kweli. Yeye aliandaa mitume kwa ajili ya utume huo. Na sasa anawatuma. Anataka wafanye kilekile ambacho Yesu mwenyewe alikuja kueneza. Hivyo, atakaye amini yale mitume watakayohubiri ataokoka, na asieamini atahukumiwa. Kadri mitume wanavyofanya ndvyio Kristo mwenyewe anafanya. Kadri mitume watakavyokataliwa ndivyo wanavyomkataa Kristo. Neno moja la tahadhari, neno kuokoka limetumika kama wakati ujao, si kwa wakati wa sasa tungali bado duniani. Bado tupo vitani, tunapambana. Kuokoka kwetu ni pale ambapo tutakuwa tumeshinda vita vya hapa duniani na kwenda huko Mbinguni. Hata mitume wenyewe wangali hapa duniani bado waliendelea kupambana kabisa na hatimaye wengi wa mitume ukimuondoa Yohane walikufa mashahidi kwa kumwaga damu yao. Tunaendelea kupambana wokovu wetu kwa sababu tayari tumeshaliamini hilo neno, lakini bado tunae shetani ambaye anatusongasonga. Tusitangaze ushindi tungali bado vitani.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo unijalie moyo hodari niweze kusimama kidete katika imani, Amina.