Aprili 24,2022 Jumapili: Jumapili ya 2 ya Pasaka

JUMAPILI YA HURUMA YA MUNGU (SHEREHE)
Nyeupe

SOMO 1: Mdo. 5:12-16

Kwa mikono ya mitume zilifanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake; hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro, akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 117:2-4, 22-27

  1. Israeli na aseme sasa,
    Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
    Mlango wa Haruni na waseme sasa,
    Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
    Wamchao Bwana na waseme sasa,
    Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele.

  1. Ulinisukuma sana ili nianguke;
    Lakini Bwana akanisadia.
    Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,
    Naye amekuwa wokovu wangu.
    Sauti ya faraha na wokovu
    Imo hemani mwao wenye haki. (K)
  2. Ee Bwana, utuokoe, twakusihi;
    Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
    Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
    Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
    Bwana ndiye aliye Mungu,
    Naye ndiye aliyetupa nuru. (K)

SOMO 2: Ufu. 1:9-11a, 12-13, 17-19

Mimi Yohane, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu. Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu, ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba. Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, “Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Basi, uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.”

SHANGILIO: Yn. 20:29

Aleluya, aleluya,
Yesu akamwambia,
Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki;
Wa heri wale wasioona, wakasadiki.
Aleluya.

INJILI: Yn. 20:19-31

Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, “Amani iwe kwenu.” Naye akiisha kusema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana. Basi Yesu akawaambia tena, “Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi.” Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Walakini mmoja wa wale Thenashara, Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana.” Akawaambia, “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.”
Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, “Amani iwe kwenu”. Kisha akamwambia Tomaso, “Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” Tomaso akajibu, akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!” Yesu akamwambia, “Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki.” Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.

TAFAKARI
TUAMINI ILI AMANI IWE NASI: Injili na masomo ya leo yanatutaka amani itamalaki kati yetu. Mitume waliwaogopa Wayahudi. Walidhani kitendo chao cha kukubali kuwa wanafunzi wa Yesu kitageuzwa jinai. Walidhani watasakwa na kuhukumiwa kwa kumfuata mhalifu. Walijua tabia za Wayahudi kuwabambikizia watu kesi na kuwaadhibu. Walijisikitikia. Walijuta kumfuasa Yesu.
Kwa hofu hii walijifungia ndani wakishangaa jinsi watakavyookoka jinai hiyo. Katika mazingira hayo ya hofu ya vichwani na moyoni iliyowafanya wajikunyate chumbani, Yesu anawajia na kuwatangazia amani. Walihitaji kuhakikishiwa amani. Kutakiwa huko aman,i kuliwachangamsha kidogo. Yesu akawaongezea matashi ya amani tena. Pamoja na kuwapatia mazingira hayo ya amani akawapa na dawa ya kutibu majeraha ya usaliti na dhambi zao na za wenzao. Ndipo aliasisi sakramenti ya Kitubio au Upatanisho mbele ya macho yao.
Mtume Tomaso aliyekosekana siku Yesu alipowamwagia mitume amani, alibaki mwana wa hofu na ukaidi. Aliposimuliwa habari za kutembelewa na Yesu mfufuka alidhihirisha kutokuwa kwake mwana wa amani. Alikaidi na kudai hataamini mpaka amwone Yesu mwenyewe na si hivyo tu bali atie mkono wake katika majeraha yake ya misumari. Dominika nyingine ilipowadia na Yesu kuwatembelea tena mitume, Tomaso alitekwa asijue la kufanya alipotakiwa akabiliane na Yesu ana kwa ana. Mkasa huu ulimpa Yesu fursa ya kumwonya Tomaso asiwe asiyeamini, bali aaminiye. Ndipo hapo Tomaso alipojibu, akimkiri Yesu kuwa Bwana wake na Mungu wake. Tomaso aliamini na kujipatia tena amani. Lakini huku akimshangaa Tomaso kwa kusadiki baada ya kuona, Yesu alitutangazia wanadamu heri ya ziada, ndiyo heri ya wasioona lakini wakasadiki. Kumbe tusadiki tupate nasi amani.
Injili inamalizikia kwa kutujulisha kwamba ishara za Yesu zilizoandikwa (sawia na zisizoandikwa) kitabuni zilikusudiwa kuwafanya watu waamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu na kwa kuamini kwao wawe na uzima kwa jina lake.
Somo la kwanza linatangaza jinsi amani inavyoweza kusambaa watu wakisadiki. Somo linataja matokeo lukuki ya kusadiki na kupata amani: kuadhimishwa na watu, kuongeza kwa idadi ya wanaoamini kwa Bwana, kuponywa kwa watu wanaosumbuliwa na maradhi mbalimbali pamoja na kufukuza pepo wachafu wanaowaudhi watu.
Somo la pili linatuhakikishia amani itakayotuvusha hadi milele. Mwandishi anasema alipopata maono ya kumwona Yesu katika utukufu wake wa mbinguni aliogopa, akaanguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Lakini Yesu alimwekea mkono wake wa kuume juu yake, akamtuliza asiogope kwa sababu yeye ni wa kwanza na wa mwisho. Ni aliye hai kwani alikuwa amekufa, na tazama, sasa alikuwa hai hata milele na milele. Aidha alimhakikishia kwamba alikuwa na funguo za mauti, na za jehanamu naye akamwagiza ayaandike mambo aliyoyaona, yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo. Kwa namna hii alisadiki na amani ikawa naye.
Tukijumlisha, tukae tukijua kwamba kumfuata kwetu Yesu si kesi ya jinai. Tukimsadiki tutajipatia amani, amani ambayo itasambaa na kuwaponya wanaogopa na kukosa amani. Watu wanaowaogopa wanasiasa wakatili, sisi tunaweza kuwapa amani. Watu wanaowaogopa matajiri wakatili, sisi tunaweza kuwapa amani. Watu wanaoogopa ushirikina sisi tunaweza kuwapa amani. Watu wanaomwogopa Shetani ovyo ovyo tunaweza kuwapa amani. Watu waliojidandishia mafundisho ya Kiislamu na dini zingine na kujitia katika hofu kubwa, mathalani, mafundisho juu ya laana, mizimu, majini, Frimasoni na kadhalika, sisi tunaweza kuwaletea amani. Tusadiki sisi kwa nguvu tujiokoe wenyewe na jirani zetu wote. Petro aliombewa na Yesu awe na imani ili kwa imani hiyo awaimarishe ndugu zake (Lk 22:31-32). Iwe vivyo kwetu.

SALA: Bwana wetu Yesu Kristo. Tunakusadiki nawe utupe amani yako. Hofu inaongezeka duniani hapa. Wanatutisha wanasiasa, watutisha wenye nguvu na kadhalika. Mafundisho holela yanatutisha pia. Tupe amani yako tufurahi katika wewe. Amina.

AAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAA