Mt. Anselmo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mdo. 3:11-26
Siku zile, kiwete yule aliyeponywa alipokuwa akiwashika Petro na Yohane, watu wote wakawakusanyikia mbio katika tao lile lililoitwa tao la Sulemani, wakishangaa sana. Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, “Enyi Waisraeli, mbona mnastaajabia haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende kwa nguvu zetu sisi, au kwa utauwa wetu sisi? Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu; ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule Mtakatifu, yule Mwenyehaki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye ilimpatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani; ambaye ilimpasa kupokewa mbinguni hata zije zamani za kufanywa upya vitu vyote, zilizonenwa na Mungu kwa kinywa cha manabii wake watakatifu tokea mwanzo wa ulimwengu. Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba: Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi. Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake. Naam, na manabii wote tangu Samweli na wale waliokuja baada yake, wote walionena, walihubiri habari za siku hizi. Ninyi mmekuwa watoto wa manabii na wa maagano yale, ambayo Mungu aliagana na baba zenu, akimwambia Ibrahimu: Katika uzao wako kabila zote za ulimwengu zitabarikiwa. Mungu, akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 8:1, 4-8
- Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyotukufu jina lako duniani mwote;
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie?
K: Ee, Mungu, Bwana wetu;
jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote.
- Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako.
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yako. (K) - Kondoo, na ng’ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni.
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za bahari, (K)
INJILI: Lk. 24:35-48
Wanafunzi waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, “Amani iwe kwenu” Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, “Mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikenishikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo.” Na baada ya kusema hayo aliwaonyesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, “Mna chakula cho chote?” Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, “Hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi, ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi.” Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, “Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo haya.”
TAFAKARI
USHAHIDI WA UFUFUKO: Katika somo la injili, tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo akiwatokea wafuasi ambao walikuwa wakishirikishana juu ya ufufuko wake. Miongoni mwao walikuwa wale wafuasi wa Emaus ambao Kristo aliwatokea na wakamtambua katika kuumega mkate. Walipokutana na wengine wakawaambia habari hizo hizo ya kwamba Kristo amefufuka. Wakati waalikuwa wanashirikishana ndipo Kristo alipotokea katikati yao na kuwatakia amani. Walishituka na kuogopa kwa sababu bado hawakuwa wanaamini na hata walipomwona wakawa wanadhani wanaona roho tu. Kristo anawathibitisha ukweli kwamba amefufuka kwa kufanya mambo ambayo roho tu hawezi akafanya. Anawaalika watazame miguu na mikono yake na wamshike. Baadaye, anakula mbele yao. Anawathibitishia kuwa ndiye Kristo Mfufuka, naye amerejea katika hali yake. Mwishowe ananukuu ushahidi wa Maandiko; ilishaandikwa kwamba yeye atakufa lakini siku ya tatu atafufuka. Sasa wafuasi wanakuwa tayari kwa utume, kumtangaza Kristo Mfufuka kwa watu wote. Ufufuko wa Kristo ndio kiini cha mahubiri ya kanisa la mwanzo. Kristo yu hai! Tunamfuata Mungu aliye hai.
SALA: Ee Kristo uliye hai, unijaze kwaa neema zako, nipate kushinda vishawishi vyangu na hatimaye niweze kuwa hai kiroho. Amina.