Aprili 19,2022; Jumanne: Jumanne ya Pasaka

Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Mdo. 2:36-41

Petro aliwaambia Wayahudi, “Nyumba yote ya Israeli na wajue yakini ya kwamba Mungu amemfanya Yesu huyo mliyemsulubisha kuwa Bwana na Kristo.” Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, “Tutendeje, ndugu zetu?” Petro akawaambia, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie.” Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, “Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukahidi.” Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu.

Wimbo wa katikati. Zab. 33:4-5,18-20, 22

 1. Neno la Bwana lina adili,
  Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
  Huzipenda haki na hukumu,
  Nchi imejaa fadhili za Bwana.

K: Nchi imejaa fadhili za Bwana.

 1. Jicho la Bwana li kwao wamchao,
  Wazingojeao fadhili zake.
  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
  Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
 2. Nafsi zetu zinamngoja Bwana;
  Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
  Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
  Kama vile tulivyokungoja Wewe. (K)

AAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAAa

INJILI: Yn. 20:11-18

Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, “Mama, unalilia nini?” Akawaambia, “Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka.” Naye akiisha kusema hayo, akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, “Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani?” Naye, huku akidhania ya kuwa ni mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.” Yesu akamwambia, “Mariamu.” Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, “Raboni!” (yaani, “Mwalimu wangu”). Yesu akamwambia. “Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu.”’ Mariamu Magdalene akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, “Nimemwona Bwana,” na ya kwamba amemwambia hayo.

TAFAKARI
UPENDO WA AJABU: Lo! Upendo wa ajabu aliokuwa nao Maria Magdalena! Hata kama wapendwa wetu tunawapenda kiasi gani, tukienda kuzika, tukiondoka basi tumeondoka. Kurudi huko labda iwe kwa ajili ya Misa ya marehemu au kubariki kaburi. Tunamwona Maria Magdalena katika injili akiwa na upendo wa ajabu kabisa. Yeye hakuridhika kuwa mbali na Bwana wetu Yesu Kristo. Alimpenda sana. Alidamka kwenda kaburini lakini hampati Kristo. Anahangaika kumtafuta Kristo alipo. Malaika wanamhoji lakini yeye anaendelea kutafuta na ndipo anakutana na Yesu. Anadhani kuwa ni mtunza bustani. Kristo anajitambulisha kwake na yeye anachanganyikiwa kwa kumwona Kristo. Bila shaka alikuwa anataka kumshika lakini Yesu akamzuia. Kwa furaha kubwa anaenda kuwapasha habari wafuasi kuwa amemwona Bwana wake anayempenda sana. Upendo wake huo mkubwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, unalipwa kwa yeye kuwa mwanadamu wa kwanza kupata habari za ufufuko. Ndiye mwanadamu wa kwanza kuanza kuihubiri Habari Njema ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tukimpenda Kristo, naye atalipa upendo wetu.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo unijalie moyo wa mapendo nikupende zaidi wewe uliye Mkombozi wangu.