Aprili 18,2022; Jumatatu: Jumatatu ya Pasaka.

Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Mdo. 2:14, 22-32

Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, “Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkasikilize maneno yangu. Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua-, mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulubisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake: Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezwa, ulimi wangu ukafurahi; tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; ukanijaza furaha kwa uso wako. Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake atamketisha pamoja katika kiti chake cha enzi; yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba Roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 16:1-2, 5, 7-11

 1. Mungu unihifadhi mimi,
  Kwa maana nakumkimbilia wewe.
  Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
  Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu;
  Wewe unaishika kura yangu.

K: Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia wewe.

 1. Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
  Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
  Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
  Ka kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. (K)
 2. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
  Nao utukufu angu unashangilia,
  Naam, mwili wangu nao utakuwa kwa kutumaini.
  Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu.
  Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. (K)
 3. Utanijulisha njia ya uzima;
  Mbele za uso wako ziko furaha tele;
  Na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele. (K)

INJILI: Mt. 28:8-15

Wanawake waliondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, “Salamu!” Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona.” Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, “Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi.” Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.

TAFAKARI
KUFIFISHA HABARI ZA UFUFUKO: Jana tumesherehekea sherehe ya Pasaka, kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ufufuko huu ni ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Wakristo wanatembea kifua mbele kwa ajili ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Bwana wetu ametushindia na hivyo ametupa sababu ya kufurahia Ukristo wetu. Lakini jambo haliwafurahishi wapinga Kristo. Katika Injili wanafanya jitihada kufififsha habari za ufufuko. Askari wanawapasha habari wakuu wa makuhani kwamba Kristo amefufuka. Nao wanaogopa kwamba habari hizi zitakuwa fedheha kwao. Wanawakusanya wazee na wanashauriana kuwawapa askari fedha ili wadanganye kwamba wanafunzi wa Yesu ndio waliomuiba wakati walinzi walipokuwa wamelala. Askari wa Kirumi walikuwa kati ya askari wenye nidhamu kabisa. Walikuwa wanatenda makosa mawili: kosa la kwanza, imekuaje Yesu aliyekuwa kaburini aibiwe? Wanaweza kutoa kisingizio kuwa walikuwa wamelala. Hili ni kosa la pili, inakuwaje askari kulala katika lindo? Maaskari wakachukua fedha na wakafanya kama walivyofundishwa. Wanaopinga ufufuko wanaendeleza uongo wakianzia na askari.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu, atujalie neema za kuendelea kupambana hapa ulimwenguni, nasi tuweze kushinda dhambi, hatimaye tuyashinde mauti, tufurahie ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo pamoja nawe mbinguni.