Aprili 15, 2022; Ijumaa: Ijumaa Kuu

Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Isa. 52:13-53 : 12

Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu), ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu. Ni nani aliyesadiki habari tuliyoileta? Na mkono wa Bwana amefunuliwa nani? Maana alikuwa mbele zake kama mche mwororo. Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zaao. Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu. Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa. Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo mbele yao wakatoa manyoya yake; naam, hakufunua kinywa chake. Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wagu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Lakini Bwana aliridhika kumchubua; Alimhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mikononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao. Kwa hiyo nitamgawia sehemu pamoja na wakuu, naye atagawanya nyara pamoja nao walio hodari; kwa sababu alimwaga nafsi yake hata kufa. Akahesabiwa pamoja na hao wakosao. Walakini alichukua dhambi za watu wengi, na kuwaombea wakosaji.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 31:1, 5, 11-13a, 14-16, 24

 1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana
  Nisiaibike milele.
  Kwa haki yako uniponye,
  Mikononi mwako naiweka roho yangu;
  Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.

K: Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

 1. Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu,
  Naam, hasa kwa jirani zangu;
  Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu;
  Walioniona njiani walinikimbia. (K)
 2. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa;
  Nimekuwa kama chombo kilichovunjika.
  Maana nimesikia masingizio ya wengi;
  Hofu ziko pande zote. (K)
 3. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
  Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
  Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
  Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
 4. Umwangaze mtumishi wako
  Kwa nuru ya uso wako;
  Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
  Iweni hodari, mpige moyo konde,
  Ninyi nyote mnaomngoja Bwana. (K)

SOMO 2: Ebr. 4:14-16; 5 : 7-9

Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. Yeye, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule, awezaye kumwokoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

INJILI: Yn. 18:1-19 : 42 (Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo)

M = Msomaji
W = maneno ya watu mbali mbali

 • = maneno ya Yesu

M. Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu yalivyoandikwa na Yohane.

Yesu anakamatwa.
M. Wakati ule Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni; palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake. Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake. Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha. Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawambia,
+ Ni nani mnayemtafuta?
M. Wao wakamjibu,
W. Ni Yesu Mnazareti.
M. Yesu akawaambia,

 • Ni mimi. M. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao. Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini. Basi akawauliza tena,
  • Mnamtafuta nani?
   M. Wakasema,
   W. Yesu Mnazareti.
   M. Yesu akajibu,
 • Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.
  M. Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao. Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi Yesu akamwambia Petro,
 • Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?

Yesu mbele ya Anasi na Kayafa, Petro anamkana Yesu.

M. Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga. Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule. Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu. Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na, mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu. Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani. Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro,
W. Wewe nawe, je! hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu?
M. Naye akasema,
W. Si mimi.
M. Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto, Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto. Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake. Yesu akamjibu,
+ Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; siku zote nalifundisha katika
sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lolote. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.
M. Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema,
W. Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?
M. Yesu akamjibu,

 • Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?
  M. Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu. Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia,
  W. Wewe nawe, je! u mwanafunzi wake mmojawapo?
  M. Naye akakana, akasema,
  W. Si mimi.
  M. Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa
  sikio na Petro; akasema,
  W. Je! mimi simekuona wewe bustanini pamoja naye?
  M. Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.

Yesu mbele ya Pilato.

M. Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri; lakini wao hawakuingia ndani ya ile Praitorio, wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka. Basi Pilato akawatokea nje, akasema,
W. Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?
M. Wakajibu wakamwambia,
W. Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.
M. Basi Pilato akawaambia,
W. Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu!
M. Wayahudi wakamwambia,
W. Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.
M. Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa. Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia,
W. Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?
M. Yesu akamjibu,

 • Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?
  M. Pilato akajibu,
  W. Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta
  Kwangu. Umefanya nini?
  M. Yesu akajibu,
 • . Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.
  M. Basi Pilato akamwambia,
  W. Wewe u mfalme basi?
  M. Yesu akajibu,
  +. Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.
  M. Pilato akamwambia,
  W. Kweli ni nini?
  M. Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia,
  W. Mimi sioni hatia yoyote kwake. Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?
  M. Basi wakapiga kelele tena kusema,
  W. Si huyu, bali Baraba.
  M. Naye yule Baraba alikuwa mnyang’anyi. Basi ndipo Pilato alipomtwaa Yesu, akampiga mijeledi. Nao askari wakamsokotea taji la miiba, wakamtia kichwani, wakamvika vazi la zambarau. Wakawa wakimwendea, wakisema,
  W. Salamu! Mfalme wa Wayahudi!
  M. Wakampiga makofi. Kisha Pilato akatokea tena nje, akawaambia,
  W. Mtu huyu namleta nje kwenu, mpate kufahamu ya kuwa mimi sioni hatia yoyote kwake.
  M. Ndipo Yesu alipotoka nje, naye amevaa ile taji ya miiba, na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia,
  W. Tazama, mtu huyu!
  M. Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema,
  W. Msulibishe! Msulibishe!
  M. Pilato akawaambia,
  W. Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake.
  M. Wayahudi wakamjibu,
  W. Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu.
  M. Basi Pilato aliposikia neno hilo akazidi kuogopa. Akaingia tena ndani ya ile Praitorio, akamwambia, Yesu,
  W. Wewe umetokapi?
  M. Lakini Yesu hakumpa jibu lolote. Basi Pilato akamwambia,
  W. Husemi nami? Hujui ya kuwa mimi nina mamlaka ya kukufungua, nami nina mamlaka ya kukusulibisha?
  M. Yesu akamjibu,
 • . Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu, kama usingepewa kutoka juu, kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako yuna dhambi iliyo kubwa zaidi.

Yesu anahukumiwa kufa.

M. Na tangu hapo Pilato akatafuta kumfungua; lakini Wayahudi wakapiga makelele wakisema,
W. Ukimfungua huyu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu ajifanyaye kuwa mfalme humfitini Kaisari.
M. Basi Pilato, aliposikia maneno hayo, akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo Sakafu ya Mawe, au kwa Kiebrania, Gabatha. Nayo ilikuwa Maandalio ya pasaka. Yapata saa sita. Akawaambia Wayahudi,
W. Tazama, Mfalme wenu!
M. Basi wale wakapiga kelele,
W. Mwondoshe! Mwondoshe! Msulibishe!
M. Pilato akawaambia,
W. Je! nimsulibishe mfalme wenu!
M. Wakuu wa makuhani wakamjibu,
W. Sisi hatuna mfalme ila Kaisari.
M. Basi ndipo alipomtia mikononi mwao ili asulibiwe; nao wakampokea Yesu.

Yesu anasulibiwa.

M. Akatoka, hali akijichukulia msalaba wake, mpaka mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, au kwa Kiebrania, Golgotha. Wakamsulibisha huko, na wengine wawili pamoja naye, mmoja huku na mmoja huku, na Yesu katikati. Naye Pilato akaandika anwani, akaiweka juu ya msalaba, imeandikwa, YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI. Basi anwani hiyo waliisoma wengi katika Wayahudi; maana mahali pale aliposulibiwa Yesu palikuwa karibu na mji; nayo iliandikwa kwa Kiebrania, na Kirumi, na Kiyunani. Basi wakuu wa makuhani na Wayahudi wakamwambia Pilato,
W. Usiandike, Mfalme wa Wayahudi; bali ya kwamba yule alisema, Mimi ni mfalme wa Wayahudi.
M. Pilato akajibu,
W. Niliyoandika nimeyaandika.

Askari wanagawanya mavazi ya Yesu.

M. Nao askari walipomsulibisha Yesu waliyatwaa mavazi yake, wakafanya mafungu manne, kwa kila askari fungu lake; na kanzu nayo. Basi kanzu ile haikushonwa, ilikuwa imefumwa yote pia tangu juu. Basi wakaambiana,
W. Tusipasue, lakini tuipigie kura, iwe ya nani.
M. Ili litimie andiko lile linenalo, Waligawanya nguo zangu, na vazi langu wakalipigia kura. Basi ndivyo walivyofanya wale askari.

Yesu na mamaye.

M. Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake,

 • Mama, tazama, mwanao.
  M. Kisha akamwambia yule mwanafunzi,
 • Tazama, mama yako.
  M. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.

Yesu anakufa

M. Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema,
+. Naona kiu.
M. Kulikuwako huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani. Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema,
+. Imekwisha.
M. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.

Yesu anatobolewa ubavu.

M. Basi Wayahudi, kwa sababu ni Maandalio, miili isikae juu ya misalaba siku ya sabato, (maana sabato ile ilikuwa siku kubwa), walimwomba Pilato miguu yao ivunjwe, wakaondolewe. Basi askari wakaenda, wakamvunja miguu wa kwanza, na wa pili, aliyesulibiwa pamoja naye. Lakini walipomjia Yesu na kuona ya kuwa amekwisha kufa, hawakumvunja miguu; lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji. Naye aliyeona ameshuhudia, na ushuhuda wake ni kweli; naye anajua ya kuwa anasema kweli ili ninyi nanyi mpate kusadiki. Kwa maana hayo yalitukia ili andiko litimie: Hapana mfupa wake utakaovunjwa. Na tena andiko lingine lanena: Watamtazama yeye waliyemchoma.

Yesu anazikwa

M. Hata baada ya hayo Yusufu na Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu (lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi), alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akauondoa mwili wake Yesu. Na Pilato akampa ruhusa. Basi akaenda, akaondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi, yapata ratili mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika. Na pale pale aliposulibiwa palikuwa na bustani; na ndani ya bustani mna kaburi jipya, ambalo hajatiwa bado mtu yeyote ndani yake. Humo basi, kwa sababu ya Maandalio ya Wayahudi, wakamweka Yesu; maana lile kaburi lilikuwa karibu.

TAFAKARI
TUMSHUKURU YESU KWA SADAKA YAKE YENYE KUFUTA KAFARA ZOTE: Wazo hili ni mwaliko unaozaliwa kutoka yote tuliyoyasikia na tunayoyatafakari leo. Mateso aliyopitia Yesu kwa ajili yetu yanafanikisha kwa asilimia mia moja ukombozi wetu. Mipango yote ya Utatu Mtakatifu kuhusu kuwarudisha wanadamu kwenye uhusiano mwema nao ilikuwa imelenga katika mapato ya sadaka la msalaba tunayoadhimisha leo. Kujimwilisha kwa Yesu kulifanyika ili sadaka ya msalaba tunayoadhimisha leo ifanikiwe. Kutwaa mwili na damu kwa Yesu Kristo kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria kulikusudiwa kufanikisha sadaka azizi ya msalaba tunayoadhimisha leo. Kilele cha sadaka ya ukombozi wetu ndiyo hiki tunachoadhimisha saa hii.
Lakini tunapofurahi kuyaorodhesha haya yote hatusemi kwamba hatuhitaji kufanya kitu chochote kwa upande wetu, la hasha. Tunatakiwa kujishirikisha katika sadaka hiyo ya ukombozi lakini si tena kupoteza muda na kafara dhalili za wanyama, ndege, vyakula na vinywaji. Kafara zote hizo zimepikuliwa na sadaka anayotutolea Yesu msalabani kama tulivyosikia kwa masikio yetu. Kujishirikisha kwetu ni kushukuru na kuishi vyema kusudi sadaka hiyo itunufaishe kwa kuingia na kupokelewa mbinguni.
Tukumbushane jinsi sadaka ya Yesu Kristo “inavyozipiga chini” sadaka na kafara zote. Ni hivi ili sadaka iwe nzuri lazima ikidhi vigezo vitatu: kitu kinachotolewa kiwe kizuri, chako mwenyewe na kitolewe kwa hiyari. Sadaka zilizokuwa zinatolewa na wanadamu katika majaribio yao ya kujipatanisha na Mungu hazikuwa zinakidhi vigezo tulivyovitaja. Nyama ya mbuzi au ya ng’ombe, au ya kuku au ya njiwa, ugali, pombe, tumbaku au pesa havikuwa vitu vyenye uzuri wa kumridhisha Mungu. Pili vitu hivyo havikuwa watoaji wala sehemu zao na tatu havikuwa vitu vinavyotolewa kwa hiyari kwa sababu watoaji hawakuwa hao wenyewe. Mbuzi, ng’ombe, kuku njiwa, ugali, tumbaku na kadhalika kimsingi vilikuwa vinalazimishwa tu kwa vile havikuwa na uhuru na hiyari ya kujitoa sadaka. Kwa namna hiyo, vitu hivi havikukidhi vigezo vya kuwa vizuri, kuwa vya watoaji wenyewe na kutolewa kwa hiyari.
Kinyume na sadaka au kafara hizo za wanadamu ni sadaka ya Yesu Kristo tunayosimuliana leo. Yesu Kristo anatoa sadaka bora kabisa kwa sababu inakidhi barabara vigezo vitatu tulivyovianisha punde. Mosi, mwili na damu anavyovitolea msalabani ni vizuri na vyenye thamani kubwa sana kwa sababu ni vya binadamu, tena Mungu – mtu. Pili ni vyake mwenyewe sio vya mtu mwingine na tatu anavitoa kwa hiyari yake mwenyewe. Kuhusu hili alisema, “Hakuna upendo mkubwa kupita huu wa mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya wengine” (Yn 15:13) na alisema anao uwezo wa kuutoa uhai wake na kuuchukua tena (Yn 10:17). Kwa kisa hiki, “Wakristo tangu mwanzo hawaachi kumsifu Yesu katika utii wake kwa Baba kuhusiana na kazi ya kutimiza mpango wa wokovu wa wanadamu wote (Flp 2:6-11).
Mateso aliyoyakubali Yesu Kristo ili kufanikisha sadaka kuu inayotosheleza yote tumeyasikia sote. Hatukosi kupata picha ya uzito na ukali wa mateso hayo. Tunapotafakari jinsi alivyobambikiziwa kesi, jinsi alivyotemewa mate, alivyopigwa makofi, alivyopigwa na mwanzi kichwani na alivyopigwa mijeledi kwa mapigo yasiyohesabika. Mijeledi ilimchubua ngozi na kumtia majeraha na alivikwa taji ya miiba kichwani. Si hivyo tu, kisha alitwishwa gogo la msalaba, alitonoswa vidonda alipokuwa anavuliwa nguo yake, alifedheheshwa kwa kuachwa uchi wa mnyama. Alipigiliwa misumari mikononi na miguuni na hatimaye alikata roho kwa uchungu. Ukitaka kupata picha simama mbele ya msalaba na ufikirie kama ungewambwa wewe pale msalabani.
Katika somo la kwanza nabii Isaya anasimulia kiutabiri habari za Yesu Kristo katika moja ya nyimbo zake nne za mtumishi wa Bwana (abed – Yahweh). Kumbe ilishatabiriwa jinsi Yesu katika kutekeleza mpango wa kuwakomboa wanadamu angalivyoonewa, huku yeye akinyenyekea na jinsi ambavyo hatafunua kinywa chake katika uonevu huo. Ilishatabiriwa jinsi angalivyofanana na mwana-kondoo apelekwaye machinjoni na angalivyonyamaza kama kondoo mbele yao wakatoa manyoya yake. Leo tumesimuliwa mubashara jinsi utabiri huo ulivyotimia na hivyo kufanikisha ukombozi wetu kwa kukatiliwa mbali na nchi ya walio hai na kwa kupigwa kwa ajili ya makosa yetu. Ndipo hapo sadaka yake ilipofana na kufuta kafara zote dhalili. Tumshukuru Mungu.
Somo la pili si habari za utabiri tena bali jinsi inavyopasa kukumbuka sadaka ya Yesu ilivyotimizwa vyema. Somo hili linatusimulia kwa shukrani jinsi Yesu katika siku za mwili wake alivyomtolea Mungu, awezaye kumwokoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi.Naye akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu na jinsi ambavyo ingawa alikuwa mwana, alivyojifunza kutii kwa mateso yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.
Tujumlishe tafakari hii kwa kukumbushana kwamba kwa jinsi Yesu alivyofanikisha kufuta kafara zote dhalili ni aibu kwetu kuziendeleza au kuzirudia. Tusihangaike tena na kafara za nyama za mbuzi, ng’ombe, kuku, pombe, tumbaku na kadhalika. Badala yake sasa tumakinike na sadaka moja tu, sadaka ya msalabani ambayo maadhimisho yake ni misa takatifu. Ya kale yameshamalizika.

SALA: Ee Yesu tunakushukuru kwa sadaka yako azizi. Tusaidie tusiendeleze wala kuzirudia sadaka na kafara zetu za zamani. Tudumishe katika sadaka yako mpya tu. Amina.