Aprili 14,2022; Alhamisi: Alhamisi Kuu: Jioni, tunaanza siku tatu kuu za mateso, kufa na kufufuka Bwana

Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Kut. 12:1-8, 11-14

Bwana akanena na Musa na Haruni katika nchi ya Misri, akawaambia, “Mwezi huu utakuwa mwanzo wa miezi kwenu; utakuwa ni mwezi wa kwanza wa mwaka kwenu. Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, ‘Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu, kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana hila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kutia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Tena mtamla hivi: mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; mimi ndimi Bwana. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri. Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu ya Bwana; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele.’”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 116:12-13, 15-18

  1. Nimrudishie Bwana nini
    Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
    Nitakipokea kikombe cha wokovu;
    Na kulitangaza jina la Bwana.

K: Kikombe kile cha baraka tukibarikicho,
Je,! Si ushirika wa damu ya Kristo?

  1. Ina thamani machoni pa Bwana
    Mauti ya wacha Mungu wake.
    Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
    Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako.
    Umevifungua vifungo vyangu. (K)
  2. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
    Na kulitangaza jina la Bwana,
    Niotaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
    Naam, mbele ya watu wake wote. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 11:23-26

Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, “Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Na vivi hivi baada ya kula akikitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.”

INJILI: Yn. 13:1-15

Basi, kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye aliwapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo. Hata wakati wa chakula cha jioni, naye Ibilisi amekwisha kumtia Yuda, mwana wa Simoni Iskariote, moyo wa kumsaliti; Yesu, hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake, na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, “Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi?” Yesu akajibu, akamwambia, “Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye.” Petro akamwambia, “Wewe hutanitawadha miguu kamwe.” Yesu akamwambia, “Kama nisipokutawadha, huna shirika nami.” Simoni Petro akamwambia, “Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia.” Yesu akamwambia, “Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote.” Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, “Si nyote mlio safi.” Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, “Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.”

TAFAKARI
KABLA YA KUFA YESU ALITUPANGIA MAMBO KWA BUSARA: Katika masomo ya leo tunaweza kukusanya mambo manne ambayo mtu mwenye busara huyafikiria na kuyapanga vyema kabla ya kufa. Mtu mwenye busara anapokufa hujitahidi kuwaachia wanaobaki nyuma yake mambo manne yafuatayo: kauli ya kuwaongoza, chakula, uongozi na nyumba ya kukaa. Mambo haya Yesu alitupangia vyema kabla ya kufa kwake. Kauli ya kutuongoza aliyotuachia ni amri ya mapendo. Chakula alichotuachia ni Ekaristi Takatifu, ambayo ni Mwili na Damu yake mwenyewe. Uongozi aliotuachia unapatikana kwa sakramenti ya upadre. Nyumba ya kukaa aliyotuachia ni Kanisa. Mambo haya manne yanajitokeza bayana katika Yn 13-17. Ndiyo kisa baada hapo Injili ya Yohane inaishia na masimulizi ya kifo na ufufuko wa Kristo tu. Inamaanisha Yesu alishamaliza kazi ya kupanga jinsi wafuasi wake watakavyoishi kabla hajaingia katika mateso yake. Alikuwa mzee wa busara hasa.
Injili yetu inatupa mfano mzuri ndani ya karamu ya mwisho. Baada ya kuwaosha miguu mitume wake, anawauliza, “Je! mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi mwaniita Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo.” Kazi ya kuwaosha wengine miguu ilikuwa kazi ya watumwa. Enzi hizo, waungwana wenye watumwa walikuwa hawagusi hata miguu yao. Waliporudi kutoka walikokuwako na miguu michafu kwa vumbi na uchafu mwingineo walikaa mahali na kunyoosha miguu yao na mtu akaja kutoa viatu na kuosha miguu ya huyo bwana wake.
Hata pale Petro anakataa kuwa Yesu, aliye mwalimu asimwoshe (asifanye kazi ya kitumwa), Yesu anamwomba akubali ili atoe funzo kuu: amri ya upendo. Yaani, wafuasi wake wajaliane kwa kila hali hata katika mambo ya kudunisha.
Somo hili lilitolewa wakati wa Karamu ya Mwisho. Mlo anaoutangaza Kristo ni Mwili na Damu yake. Kwa kauli yake ya kuwataka mitume wafanye na wale mwili na wanywe damu ya Yesu aliwabainisha mitume kuwa viongozi wa Kanisa. Kuweka chakula hicho kipya mikononi mwa mitume, moja kwa moja tunapewa sakramenti mbili: Ekaristi Takatifu na Upadre. Tayari Yesu alishamaliza kupanga mambo matatu kati ya manne yaliyotakiwa kupangwa kwa ajili ya wote watakaomfuata: amewapatia kauli ya kuwaongoza, kuwahakikishia chakula na kuwaratibia nani wa kuwaongoza. Mintarafu jambo la nne ndiyo nyumba ya kukaa ndiyo jambo aliloliweka bayana kwa uratibisho wa kanisa moja katika sala na matashi yake katika Yn 17:11.21.
Somo la kwanza leo, linatufunulia busara ya Mungu katika kuwapangia watu chakula. Mungu aliwapa Waisraeli mpango wa kuila pasaka na mwanakondoo wa pasaka. Huu ni mwanzo uliodokeza Ekaristi Takatifu, chakula cha kututosha tunaosafiri kumkimbia Shetani tukielekea mbinguni. Heko Bwana wetu kwa kutupangia vyema. Sasa tumeelewa.
Somo la pili ndilo linfanya muhtasari wa jinsi Sakramenti za Ekaristi Takatifu na Upadre zilivyowekwa kwa ajili ya lishe na uongozi katika Kanisa la Mungu. Muhtasari huu unasimuliwa kwa Wakorintho lakini kwa niaba yetu sote. Sasa imekuwa wazi zaidi. Tunashukuru kwa kuelewa tena.
Kwa kumalizia, ikiwa tumegundua jinsi Yesu Kristo alivyokufa kama mzee mwenye busara kwa kutuhakikishia kauli ya kutuongoza, chakula, na nyumba ya kukaa, tunatakiwa mambo mawili ya msingi. Tuwe wenye shukrani, tumshukuru siku zote na kudumu katika kunufaika nayo. Hakuna dhiki ya kutangatanga nje ya hayo na nje ya Kanisa la Bwana. Tusiwe tena watu wanatoka katika familia nzuri na kwenda mitaani kuishi kama chokoraa.

SALA: Ee Yesu Kristo, tunakushukuru kwa kutupenda na kufikiria matunzo yetu ya kiroho. Tunakushuru kwa sakramenti za Ekaristi Takatifu na upadre, kauli ya upendo ya kuongozea maisha yetu na Kanisa nyumba yetu ya kuishi ndanimwe. Amina.