Aprili 13,2022; Jumatano: Juma Kuu.

Mt. Martino I, Baba Mt. Shahidi
Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Isa. 50:4-9

Bwana Mungu amenipa ulinzi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemea kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?

Wimbo Wa Katikati: Zab. 69:7-9, 20-21, 30, 32-33

 1. Kwa ajili yako nimestahimili laumu
  Fedheha imenifunika uso angu.
  Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
  Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
  Maana wivu wa nyumba yako umenila,
  Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.

K: Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.

 1. Laumu imenivunja moyo,
  Nami ninaugua sana.
  Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;
  Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu..
  Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
  Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. (K)
 2. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
  Nami nitamtukuza kwa shukrani.
  Walioonewa watakapoona watafurahi;
  Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
  Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
  Wala hawadharau wafunga wale. (K)

INJILI: Mt. 26:14-25

Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, “Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu?” Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, “Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?” Akasema, “Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, ‘Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.’” Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, “Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.” Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, “Ni mimi, Bwana?” Akajibu akasema, “Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.” Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, “Ni mimi, Rabi?” Akamwambia, “Wewe umesema.”

TAFAKARI
OLE WAKE MSALITI: Leo msaliti anaonekana wazi akienda kwa wakuu wa makuhani na kuomba kitu ili aweze kumsaliti Kristo. Nao wanampa vipande thelethini vya fedha. Tangu pale, anatafuta nafasi ya kumsaliti Kristo. Wakila karamu ya mwisho, Kristo anatabiri tena juu ya msaliti, na msaliti anatapatapa hata na kuuliza, “Ni mimi Bwana?” Kristo anamjibu vilivyo. Mitume wanahuzunika sana. Yesu huhuzunika sana tunapomsaliti. Kwake Yuda, Yesu anahiari asingalizaliwa. Bora kutozaliwa, kuliko kuzaliwa na kuwa msaliti. Usaliti ni mbaya wapendwa. Tunavyoendelea kumsaliti Kristo, Kristo anasema ni bora tusingalizaliwa. Ni hasara kuzaliwa halafu ukawa msaliti kwa wengine. Katika maisha yetu daima tupambane kuhakikisha kuwa hatupo miongoni mwa wasaliti. Tuenende kadri ya mafundisho ya Kristo na kadri ya maelekezo yake. Tunavyofanya hivyo tutakuwa kweli wana warithi wa ufalme wa Mungu. Hata hivyo, kinyume chake tunakuwa wasaliti na tunaishi maisha ya hasara! Kuliko kuwa msaliti, bora usizaliwe kabisa.

SALA: Ee Mwenyezi Bwana wetu, unipe moyo mnyoofu. Uniepushe na usaliti.