Aprili 11,2022 Jumatatu: Juma Kuu

Mt. Stansilao, Askofu wa Shahidi
Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Isa. 42:1-7

Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda, yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake, yeye awapaye pumzi watu walio juu yake, yeye awapaye roho wao waendao ndani yake. “Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 27:1-3, 13-14

 1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
  Nimwogope nani?
  Bwana ni ngome ya uzima wangu,
  Nimhofu nani?

K: Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

 1. Watenda mabaya waliponikaribia,
  Wanile nyama yangu,
  Watesi wangu na adui zangu,
  Walijikwaa wakaanguka. (K)
 2. Jeshi lijapojipanga kupigana nami,
  Moyo wangu hautaogopa.
  Vita vijaponitokea,
  Hata japo nitatumaini. (K)
 3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
  Katika nchi ya walio hai.
  Umngoje Bwana, uwe hodari,
  Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

INJILI: Yn. 12:1-11

Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alifika Bethania, alipokuwapo Lazaro, yeye ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Basi wakamwandalia karamu huko; naye Martha akatumika; na Lazaro alikuwa mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye. Basi Mariamu akatwaa rali ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi, akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu. Basi Yuda Iskariote, mmojawapo wa wanafunzi wake, ambaye ndiye atakaye kumsaliti, akasema, “Mbona marhamu hii haikuuzwa kwa dinari mia tatu, wakapewa maskini?” Naye aliyasema hayo, si kwa kuwahurumia maskini; bali kwa kuwa ni mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akavichukua vilivyotiwa humo. Basi Yesu alisema, “Mwache aiweke kwa siku ya maziko yangu. Kwa maana maskini mnao siku zote pamoja nanyi; bali mimi hamnami siku zote.” Basi watu wengi katika Wayahudi walipata kujua ya kuwa yeye yuko huko; nao wakaja, si kwa ajili yake Yesu tu, ila wamwone na Lazaro, ambaye Yesu alimfufua katika wafu. Nao wakuu wa makuhani wakafanya shauri la kumwua Lazaro naye; maana kwa ajili yake wengi katika Wayahudi walijitenga, wakamwamini Yesu.

TAFAKARI
YESU NI WA THAMANI: Katika Juma Kuu tunatafakari mateso ya Bwana wetu Yesu Kristu. Kristu yupo na mitume wake kabla ya kukamatwa. Wapo mezani katika familia ya Maria, Martha na Lazaro, Maria anachukua mafuta ya thamani nyingi anampaka Yesu miguuni halafu anamfuta miguu kwa nywele zake. Kitendo hicho kinafanya harufu nzuri ijae humo ndani na Yuda anaona hizo fedha zimepotea bure. Anashauri heri mafuta yangeuzwa, na pesa wakapewa maskini. Kristo anasema kwamba maskini tunao siku zote.
Kristo tayari anabashiri maziko yake. Yeye ni wa thamani na anastahili kufanyiwa vitu vya thamani ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwepo wake kati yetu. Wapendwa, tunapotafakari mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, tukumbuke kwamba Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Je, tunathamini kwa kiasi gani hicho alichokifanya Kristo? Sisi tunalo la kumrudishia Kristo? Lazima nalo liwe la thamani. Tukitafakari mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo, tutafakari na kuona namna Bwana wetu Yesu Kristo alivyo wa thamani.

SALA: Ee Bwana wa thamani, unijalie niyathamini maisha yangu yaliyokombolewa kwa damu yako ya thamani.