Aprili 10,2022; Jumapili : Jumapili ya Matawi na Kumbukumbu ya Historia ya Mateso ya Bwana

INJILI: Lk. 19:28-40

Wakati ule Yesu alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu. Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi, akisema, “Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa. Na kama mtu akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Semeni hivi, ‘Bwana ana haja naye’”. Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia. Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, “Mbona mnamfungua mwana-punda?” Wakasema, “Bwana ana haja naye.” Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu. Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani. Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, “Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu!” Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, “Nawaambia ninyi, wakinyamaza haya mawe yatapiga kelele.”

SOMO 1: Isa. 50:4-7

Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 22:7-8, 16-17a; 18-19; 22-23

 1. Wote wanionao hunicheka sana
  Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
  Husema, “Umtegemee Bwana; na amponye;
  Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.”

(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

 1. Kwa maana mbwa wamenizunguka;
  Kusanyiko la waovu wamenisonga;
  Yamenizua mikono na miguu.
  Naweza kuihesabu mifupa yangu yote.
 2. Wanagawanya nguo zangu,
  Na vazi langu wanalipigia kura.
  Nawe, Bwana, usiwe mbali,
  Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. (K)
 3. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
  Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
  Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni
  Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni. (K)

SOMO 2: Flp. 2:6-11

Yesu mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

SHANGILIO: Flp 2:8-9

Kristo alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina.

HISTORIA YA MATESO YA BWANA

TAFAKARI
YESU ALIJIFANYA PELIKANE ILI NDUGU ZAKE TUPONE: Tukitafakari kwa nini Yesu alikubali mateso yote hayo tuliyosimuliwa tunafikia kwenye wazo hili kwamba alijifanya mwenyewe pelikane ili ndugu zake tupone. Pelikane ni ndege wa ajabu kabisa anapokuja katika suala la kulisha vifaranga wake. Ukame unapobamba na njaa kutishia uhai wa vifaranga wake huruhusu damu yake inyonywe na wanawe. Kwa namna hii huuweka uhai wake rehani ilmradi awaokoe watoto wake. Uamuzi huu na majitoleo hayo ndiyo tunayoweza kulinganisha na anachotufanyia Yesu leo. Yupo tayari kutolea uhai wake kwa ajili yetu sisi ndugu zake. Tumshukuru kwa majitoleo hayo ya ajabu.
Kujifanya kwake pelikane kunaanzia kwenye kukubali kwake kuachilia utukufu wake wa kimungu na kujimwilisha, akaishi kati yetu na akapaswa kuyakabili mateso kama tulivyosimuliwa leo. Mateso ya Yesu yalikuwa yote ya kisaikolojia na ya kimwili. Kisaikolojia Yesu aliteseka katika kujua kwamba anaowasaidia ndiyo wanaomkataa. Alitiwa majonzi kuwaona watu wakipenda giza na kukataa mwanga. Alisikitishwa kushuhudia walio wake wakimkataa. Aidha ilimsikitisha sana kuona alivyobambikiwa kesi na kuhukumiwa bila kufuata sheria yote, ikiwamo kuburuzwa mahakamani usiku kuchwa na baadaye kuhukumiwa kifo kwa makosa yasiyo na uzito wa adhabu hiyo.
Kimwili Yesu aliumizwa mno. Alitemewa mate, alipigwa makofi, alipigwa na mwanzi kichwani na alipigwa mijeledi kwa mapigo yasiyohesabika. Mijeledi ilimchubua ngozi na kumtia majeraha na alivikwa taji ya miiba kichwani. Si hivyo tu, kisha alitwishwa gogo la msalaba, alitonoswa vidonda alipokuwa anavuliwa nguo yake, alifedheheshwa kwa kuachwa uchi wa mnyama, alipigiliwa misumari mikononi na miguuni na hatimaye alikata roho kwa uchungu. Ukitaka kuonja uchungu wa mateso haya vaa viatu vyake.
Lakini mateso haya na vinaganaga vyake ndiyo kilele cha kujifanya kwake pelikane. Kutangaza upelikane wa Yesu Kristo, mtume Petro anaandika, “Hayo ndiyo mliyoitiwa maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili mfuate mwenendo wake. Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika midomoni mwake. Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki. Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa” (1Pet 2:21-24).
Somo la kwanza linatangaza vyema jinsi Yesu alivyojifanya pelikane kwa ajili yetu. Tunasoma jinsi ambavyo kwa ajili yetu hakuwa mkaidi, wala kurudi nyuma. Tunaambiwa aliwatolea wapigao mgongo wake, na wang’oao ndevu mashavu yake; hakuficha uso wake usipate fedheha na kutemewa mate. Alipojitosa katika adha hizo tumaini lake lilikuwa katika Bwana Mungu ambaye angemsaidia; hivyo hakutahayari, akakaza uso wake kama gumegume, naye hakuona haya hata kidogo.
Na somo la pili nalo linajazia maelezo. Linasema yeye ambaye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wetu sisi wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Tukijumlisha maneno yetu tujigeukie wenyewe. Baada ya kusimuliwa jinsi Yesu Kristo alivyojifanya pelikane kwa ajili yetu, kwa upande wa Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina na kwa upande wetu tunawiwa shukrani ndiko goti la kila kitu kichopo mbinguni, duniani, na chini ya nchi kupigwa kwa jina la Yesu, na kila ulimi kukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

SALA: Ee, Mungu tusaidie kuitambua kwa shukrani sadaka aliyoitoa Mwanao kama pelikane kwa ajili yetu. Tuchunge tusiipuuze wala kuisahau. Amina.