Aprili 8, 2022;Ijumaa: Juma la 5 la Kwaresma

Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Yer. 20:10-13

Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, “Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.” Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana kwa maana ameiponya roho ya mhitaji katika mikono ya watu watendao maovu.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 18:1-6

  1. Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
    Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu
    Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
    Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
    Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa,
    Hivyo nitaokoka na adui zangu.

K: Katika shida yangu nalimwita Bwana,
Akaisikia sauti yangu.

  1. Kamba za mauti zilinizunguka,
    Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
    Kamba za kuzimu zilinizunguka,
    Mitego ya mauti ikanikabili. (K)
  2. Katika shida yangu nalimwita Bwana,
    Na kumlalamikia Mungu wangu.
    Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
    Kilio changu kikaingia masikioni mwake. (K)

INJILI: Yn. 10:31-42

Wayahudi waliokota mawe ili wampige. Yesu akawajibu, “Kazi njema nyingi nimewaonyesha, zitokazo kwa baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe?” Wayahudi wakamjibu, “Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.” Yesu akawajibu, “Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; -na maandiko hayawezi kutanguka-, je! yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, ‘Unakufuru’; kwa sababu nalisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu’? Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba.” Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohane akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. Na watu wengi wakamwendea, wakasema, “Yohane kweli hakufanya ishara yoyote, lakini yote aliyoyasema Yohane katika habari zake huyu yalikuwa kweli.” Nao wengi wakamwamini huko.

TAFAKARI
YESU NI MWANA WA MUNGU: Wayahudi wanaokota mawe wampige Kristo ati amekufuru kwa kujiita mwana wa Mungu. Wao wanamuona yeye ni mwanadamu tu. Waswahili wanasema, mtoto wa nyoka ni nyoka, kwa hiyo mwana wa Mungu ni Mungu. Bwana wetu Yesu Kristo anajenga hoja kwamba yeye kweli ni Mungu. Kwanza, Maandiko Matakatifu yanatambua na kumpa hadhi mwanadamu kuwa Mungu. Ama ndivyo, sembuse yeye ambaye Mwenyezi Mungu ndiye amemtakasa na kumtuma ulimwenguni! Pili, tutazame kazi alizozitenda. Hizo, zinaonyesha wazi kwamba, Baba yu ndani yake naye yu ndani ya Baba. Kwa mantiki hiyo yeye na Baba ni wamoja, Kristo ni Mungu kweli na mtu kweli. Yeye ni Mungu kweli kwa asilimia mia moja, na mwanadamu kweli asilimia mia moja. Haya mawili yanasababisha ukombozi wa mwanadamu. Sisi tunaojua kwamba Kristo ni Mwana wa Mungu, tujitahidi kuwa na imani hai kwake, na tuwaelekeze wengine wamtambue Kristo, Mwana wa Mungu ambeye ni Mungu. Bila kuhangaika, tumfuate Mkombozi wetu, aliye uzima na wokovu wetu.

SALA: Ee Yesu Mwana wa Mungu, utuzidishie imani kwako, tukukiri na kukusikiliza wewe Mkombozi wetu.