Aprili 7 Alhamisi: Juma la 5 la Kwaresma

Mt. Yohane Baptista wa Salle, Padre
Kumbukumbu
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mwa. 17:3-9

Abramu akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, “Mimi, agano langu nimefanya nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu, lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi. Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu kwako na kwa uzao wako baada yako, nami nitakupa wewe na uzao baada yako nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami nitakuwa Mungu wao.” Mungu akamwambia Ibrahimu, “Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.”

Wimbo wa katikati: Zab. 105:4-9

 1. Mtakeni Bwana na nguvu zake,
  Utafuteni uso wake siku zote.
  Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,
  Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.

K: Analikumbuka agano lake milele.

 1. Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;
  Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
  Yeye, Bwana, ndiye Mungu wetu;
  Duniani mwote mna hukumu zake. (K)
 2. Analikumbuka agano lake milele;
  Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.
  Agano alilofanya na Ibrahimu,
  Na uapo wake kwa Isaka. (K)

INJILI: Yn. 8:51-59

Yesu aliwaambia Wayahudi, “Amin, amin, nawaambia, Mtu akilishika neno langu, hataona mauti milele. Basi Wayahudi wakamwambia, Sasa tumeng’amua ya kuwa una pepo. Ibrahimu amekufa, na manabii wamekufa; nawe wasema, Mtu akilishika neno langu, hataonja mauti milele. Wewe u mkuu kuliko baba yetu Ibrahimu, ambaye amekufa? Nao manabii wamekufa. Wajifanya u nani”? Yesu akajibu, “Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu; anitukuzaye ni Baba yangu, ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu. Wala ninyi hamkumjua; lakini mimi namjua. Nikisema ya kwamba simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi; lakini namjua, na neno lake nalishika. Ibrahimu, baba yenu, alishangilia kwa vile atakavyoiona siku yangu; naye akaiona, akafurahi.” Basi Wayahudi wakamwambia, “Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?” Yesu akawaambia, “Amin, amin, nawaambia: Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.” Basi wakaokota mawe ili wamtupie; lakini Yesu akajificha, akatoka hekaluni.

TAFAKARI
KABLA YA IBRAHIMU YESU YUPO: Katika Kanuni ya Imani tunasali kwamba, Yesu alizaliwa kwa Baba tangu milele yote. Katika Umungu wake na katika Nafsi yake ya Pili ya Mungu, yeye ni wamilele, lakini katika ubinadamu wake alizaliwa wakati fulani. Katika somo la injili Wayahudi wanaona kwamba Baba yao Ibrahimu ni mkubwa kuliko Kristo. Kristo anawaambia kuwa wakilishika neno lake hawataona mauti milele. Hilo linawachanganya. Wanamuuliza kana kwamba Kristo ni mkubwa kuliko Ibrahimu amabaye amekufa au manabii ambao wamekufa? Yesu anawaambia kwamba hatajitukuza bali Mwenyezi Mungu mwenye atamtukuza. Ndipo anapowaambia kwamba Ibrahimu alishangilia kuiona siku yake na akafurahi. Pengine kipindi kile alikuwa na miaka Thelathini hivi, anawezaje sasa kumfahamu Ibrahimu. Lakini yeye anawaambia kabla ya Ibrahimu kuwako yeye alikuwepo. Kristo ni wa milele. Katika Nafsi yake ya Pili yeye ni Mungu na hana mwanzo wala mwisho. Tufahamu hayo na tujue kwamba tunapojongea mbele yake, tunaenda mbele ya Mungu ambaye yupo wakati wowote. Tumwendee kwa imani, tukijua anatupenda.

SALA: Ee Bwana wa milele yote, utupokee waja wako tuombapo msaada wako.