Aprili 6,2022 Jumatano: Juma la 5 la Kwaresma

Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Dan. 3: 14-20, 91-92, 95

Nebukadreza, aliwaambia, “Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! Ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? Basi sasa, kama mkiwa tayari wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakaye waokoa ninyi na mikono yangu?” Ndipo Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakajibu, wakamwambia mfalme, “Ee Nebukadreza, hatuna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha”. Ndipo Nebukadreza akajaa ghadhabu, na sura ya uso wake ikabadilika juu ya Shadraka, na Meshaki na Abednego, basi akatoa amri watie moto ile tanuru mara saba kuliko desturi yake ya kutiwa moto. Kisha akawaamuru baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake kuwafunga Shadraka, na Meshaki, na Abednego, na kuwatupa katika ile tanuru iliyokuwa ikiwaka moto. Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, “Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto?” Wakajibu, wakamwambia mfalme, “Kweli, Ee mfalme.” Akajibu, akasema, “Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.” Nebukadreza akanena, akasema, “Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego; aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu ila Mungu wao wenyewe.”

Wimbo Wa Katikati: Dan. 3:52-56

 1. Umehimidiwa, Ee Bwana, Mungu wa baba zetu;
  Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
  Limehimidiwa jina lako takatifu, tukufu;
  Lastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.

K: Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.

 1. Umehimidiwa katika hekalu la fahari yako takatifu;
  Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
  Umehimidiwa juu ya kiti cha ufalme wako;
  Watahili kusifiwa na kuadhimishwa milele. (K)
 2. Umehimidiwa utazamaye vilindi, uketiye juu ya makerubi
  Wastahili kusifiwa na kuadhimishwa milele.
  Umehimidiwa katika anga la mbinguni
  Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele. (K)

INJILI: Yn. 8: 31-42

Yesu aliwaambia wale Wayahudi waliomwamini, “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” Wakamjibu, “Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, ‘Mtawekwa huru?”’ Yesu akawajibu, “Amin, amin, nawaambia: Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi. Wala mtumwa hakai nyumbani siku zote; mwana hukaa siku zote. Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. Najua ya kuwa ninyi ni uzao wa Ibrahimu; lakini mnatafuta kuniua kwa sababu neno langu halimo ndani yenu. Niliyoyaona kwa Baba ndiyo niyanenayo; nanyi vivyo hivyo mliyoyasikia kwa baba yenu ndiyo myatendayo.” Wakajibu, wakamwambia, “Baba yetu ndiye Ibrahimu!” Yesu akamwambia, “Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi, mtu ambaye nimewaambia iliyo kweli, niliyoisikia kwa Mungu. Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu.” Ndipo walipomwambia, “Sisi hatukuzaliwa kwa zinaa; sisi tunaye Baba mmoja, yaani, Mungu.” Yesu akawaambia, “Kama Mungu angekuwa baba yenu, mngenipenda mimi; kwa maana nalitoka kwa Mungu, nami nimekuja; wala sikuja kwa nafsi yangu, bali yeye ndiye aliyenituma.”

TAFAKARI
UKWELI UTATUWEKA HURU: Je, ukweli ni nini? Pilato alimwuliza Bwana Yesu na Yesu hakumpatia jawabu. Ukweli ni ukubaliano kati ya fikra na kitu halisi. Kwa mfano unaposema kwamba hiki ni kikombe itakuwa kweli kama hicho kitakuwa kweli ni kikombe lakini ikiwa sivyo basi itakuwa sio ukweli. Mwanadamu katika maisha yake amehangaika akitaka kuufahamu ukweli. Mwenyezi Mungu ametuumba namna hii tusumbuke, tuhangaike, tupambane kuutafuta ukweli, na ni katika kuutafuta ukweli ndipo Mungu anatusogeza karibu naye. Katika Injili Bwana wetu Yesu Kristo anawaambia Wayahudi kwamba wakilisikia neno lake, watakuwa wanafunzi wake wa kweli tena wataifahamu kweli na hiyo kweli itawaweka huru. Tukilisikia neno lake tutapata mafundisho ambayo yametoka kwa kweli. Yesu Kristo ni ukweli, nayo mafundisho yake ni kweli, Tukiyashika, tunakuwa huru. Kuupata ukweli, kuusikiliza, na kuufuata, ndiko kuwa huru. Tusiyasikilize mafundisho potovu. Tumeujua ukweli, tusimame katika ukweli, tukibaki kuwa huru. Sisi si watumwa na hatuna sababu ya kutanga tanga.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu utujalie neema tunazohitaji kwa ajili ya kuendelea kudumu katika ukweli uliofunuliwa na Bwana wetu Yesu Kristo.