Aprili 5,2022; Jumanne: Juma la 5 la Kwaresma.

Mt. Vinsenti Ferrer, Padre
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Hes. 21: 4-9

Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, “Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.” Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

Watu wakamwendea Musa, wakasema, “Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa.” Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, “Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi.” Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikawa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 102:1-2, 15-20

 1. Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,
  Kilio changu kikufikie.
  Usinifiche na uso wako siku ya shida yangu,
  Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.

K: Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,
Kilio changu kikufikie.

 1. Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
  Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
  Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
  Atakapoonekana katika utukufu wake,
  Asiyadharau maombi yao. (K)
 2. Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
  Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
  Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
  Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
  Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)

INJILI: Yn. 8: 21-30

Yesu aliwaambia Mafarisayo, “Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja.” Basi Wayahudi wakasema, “Je! atajiua! Kwa kuwa asema, ‘Mimi niendako ninyi hamwezi kuja’?” Akawaambia, “Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; Kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu.” Basi wakamwambia, “U nani wewe?” Yesu akawaambia, “Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake ndiyo ninenayo katika ulimwengu.” Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. Basi Yesu akawaambia, “Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniancha peke yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo.” Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamini.

TAFAKARI
MUNGU KUTOKA KWA MUNGU: Katika Injili, Yesu anaongea na Mafarisayo ambao inavyoonekana, hawamfahamu. Ndipo Kristo anawaambia ataondoka nao watamtafuta wasimuone. Tena anasema watabaki katika dhambi zao, naye anapoenda hawawezi kupajua. Swali wanalojiuliza ni, “Atajiua?” Kristo anapata wakati mgumu kukubalika kwa Mafarisayo ambao wamekaza shingo zao wakikataa kumkubali kuwa ni Mwana wa Mungu na ametumwa na Mungu. Lakini Kristo hataki kutumia nguvu kuwashawishi. Anawaambia kwamba wakishakumwinua ndipo watafahamu Kristo ni nani. Hili linatokea kweli kwani baada ya Kristo kufa msalabani mmoja wa Maakida alikiri kuwa Kristo kweli alikuwa Mwana wa Mungu. Lakini, baada ya kupaa mbinguni Kristo anawaagiza Mitume kumhubiri kwa watu wote, tukio ambalo linafanya watu waendelee kumkiri na kufahamu kuwa kweli, Kristo alikuwa Mwana wa Mungu. Sisi tuliobahatika kufahamu siri za umungu wa Kristo tuna kila sababu ya kufundisha wengine kumfahamu Kristo kama Mwana wa Mungu. Mungu kutoka kwa Mungu.

SALA: Ee Yesu Mwana wa Mungu utujalie nguvu ya kuweza kukuhubiri wewe kwa watu wasiokujua bado na hivyo ulimwengu ukufahamu wewe.