SOMO 1: Isa. 43: 16-21
Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari, na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi. “Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani! Tazama, nitatenda neno jipya: sasa litachipuka je, hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni, kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 126
- Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko.
Na ulimi wetu kelele za furaha.
K: Bwana alitutendea mambo makuu, Tulikuwa tukifurahi.
- Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K) - Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi
Watavuna kwa kelele za furaha. (K) - Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)
SOMO 2: Flp. 3: 8-14
Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.
SHANGILIO: Yoe. 2:12, 13
Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote,
Kwa maana ni mwenye rehema na huruma
INJILI: Yn. 8: 1-11
Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, “Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?” Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.” Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, “Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?” Akamwambia, “Hakuna Bwana.” Yesu akamwambia, “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.”
TAFAKARI
MUNGU HAJAKATA TAMAA NA SISI: Mungu anataka tuwe tunasahau mambo ya zamani na kuanza upya. Mkasa uliompata mwanamke anayesimuliwa katika Injili na jinsi Yesu alivyoshughulikia kesi yake ndio unaotoa wazo hili. Kwa ujumla, Mungu hakati tamaa na mtu yeyote hata yule anayehesabiwa na watu mwovu sana. Mungu hakukata tamaa na mwanamke mzinzi wala na washtaki wake ambao walikuwa wadhambi vile vile. Kwa wema wake aliwatengenezea wote fursa ya kutubu na kurudi kwake.
Wayahudi walitafsiri amri ya sita ya “Usizini” kwa kuisisitiza zaidi kwa wanawake. Hivyo wanaume waliona amri hiyo inawahusu zaidi akina mama wakati wao walijihusisha zaidi na amri ya tisa, yaani ile ya “Usitamani mke asiye wako”. Waliwalazimisha akina mama waishike sana amri ya sita kusudi kusiwe na utata katika baba mzazi wa mtoto. Wanaume wenyewe walijirahisishia maisha kwa kubagua hatia ya uzinzi. Walisema mwanaume Myahudi alipolala na mwanamke asiye Myahudi hakukuwa na hatia ya uzinifu. Aidha walisema alipolala na mtumwa haikuwa uzinifu. Inaonekana wengine walitaka isiwe pia hatia ikiwa mwanaume Myahudi analala na mwanawake aliyeachika au mjane.
Basi, fumanizi la mwanamke aliyeolewa ilikuwa mkasa mbaya sana kwa mwanamke mhusika. Sheria ya Musa iliamuru watu wanaofumaniwa wapigwe mawe (Kum 22:22), hata hivyo kimsingi walimwang’azia macho zaidi mwanamke. Ndiyo maana katika Injili wanaomleta mwanamke aliyefumaniwa hawasikiki wakishughulika sana na mwanaume aliyehusika naye. Kama hakuwazidi nguvu katika kukimbia basi sababu ni hii, fumanizi lilikuwa shauri ndogo kidogo kwa mwanaume. Lawama na hatia ilikuwa zaidi kwa mwanamke.
Waliofumania uzinzi ule wa asubuhi walijua adhabu iliyoainishwa katika torati. Walikuja kwa Yesu kupima kina cha uelewa na ushikaji wake sheria ya Musa. Kumbe walipokuwa wanasubiri Yesu awaunge mkono katika kutekeleza hukumu ya kumwangamiza kwa mawe mwanamke mzinzi, Yesu akatumia fursa hiyo kuzigonga dhamiri zao. Alichokoza dhamiri zao kwa kuwataka asiye na dhambi aokote jiwe amtupie mdhambi waliyemleta. Alipokuwa anawasubiri watafakari alichowaomba, akawa anaandika andika chini. Hatujui alichokuwa anakiandika. Kijulikane kisijulikane alichokuwa anaandika ndivyo alikuwa muda kwa wakosefu kujihukumu wenyewe.
Somo la kwanza linaeleza vizuri wazo letu la Mungu kutokata tamaa na mtu yeyote. Mungu anawakumbusha Wayahudi kwamba hali yao ilikuwa mbaya huko Misri lakini aliwaokoa na kuwapitisha jangwani hadi mahali salama katika nchi ya ahadi. Kwa ukarimu huo aliowafanyia wanapaswa kusahau historia hiyo mbaya na kuanza maisha mapya ya kiuadilifu. Kifupi, anawaambia yuko tayari kuanza pamoja nao maisha yanayoelekea kwenye uzima wa milele ilmradi na wao wawe tayari na watoe ushirikiano.
Katika somo la pili, Paulo anajieleza vizuri jinsi alivyounganishwa katika mchakato wa kutafuta upya katika Mungu. Akipitisha kichwani mwake hali yake ya mwanzo anaiona vyema safari yake mpya. Ndipo anapotangaza kwamba hadhanii nafsi mwake kwamba ameshashika mede isipokuwa anatenda neno moja tu; kuyasahau yaliyo nyuma yake, kuyahesabu mavi tu, akiyachuchumilia yaliyo mbele yake; kukaza mwendo, aifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.
Tukijumlisha, tunaalikwa na Mungu tuishi kwa falsafa ya “Yaliyopita si ndwele, tuyagange yaliyomo na yajayo.” Yeye hajakata tamaa na mtu yeyote, sisi tusikate tamaa wenyewe.
SALA: Ee, Mungu mwema, tunaomba utupe nguvu ya kutazama mbele. Magumu na mapungufu maishani mwetu yasilegeze hamasa ya kutafuta kufika kwako kusudi tukae pamoja nawe na watakatifu wako. Amina.