Mt. Fransisko wa Paulo, Mweremita
Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Yer. 11: 18-20
Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 7:1-2, 8-12
- Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,
Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,
Akiivunja vunja pasipokuwa na wa kuponya.
K: Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe.
- Bwana, unihukumu mimi,
Kwa kadiri ya haki yangu,
Sawasawa na unyofu nilio nao.
Ubaya wao wasio haki na ukome,
Lakini mthibitishie mwenye haki. (K) - Ngao yangu ina Mungu,
Awaokoaye wanyofu wa moyo.
Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)
INJILI: Yn. 7: 40-52
Wengine katika mkutano walipoyasikia maneno ya Yesu, walisema, “Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, “Huyu ndiye Kristo.” Wengine wakasema, “Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi?” Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, “Mbona hamkumleta?” Wale watumishi wakajibu,” Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena.” Basi Mafarisayo wakawajibu, “Je! ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo?” Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), “Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo?” Wakajibu, wakamwambia, “Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.”
TAFAKARI
NABII TOKA GALILAYA: Wayahudi wanataka kumuua Yesu. Wanatafuta kila sababu itakayowapa uhalali wa kufanya hivyo wanakosa. Hata wanatuma watu kumkamata na watu hao wanashindwa kwa vile walishuhudia jinsi Yesu alivyoongea na wao wakaamini. Sasa hoja iliyobaki ni kuwa Kristo alitoka Galilaya na hiyo ilitosha kumuondolea uhalali wa kuwa nabii. Lakini hoja hiyo pia haina mashiko kwa vile Kristo alizaliwa Betlehemu ya Uyahudi. Kwa nini sasa Kristo anaonekana kama ni Mgalilaya? Ni kwa vile wazazi wake waliishi na kuendesha maisha yao huko. Malaika Gabrieli alipotumwa kumpasha habari Maria za kuzaliwa Mkombozi Maria alikuwa akiishi Galilaya. Lakini Maria alipokaribia kujifungua walipanda kwenda Jerusalemu na mumewe kwa ajili ya kujiorodhesha katika sensa iliyoamuriwa na utawala wa Kirumi. Alipokuwa huko ndipo alipojifungua mwanawe. Herode alipotaka kumuua mtoto, familia ilikimbilia Misri. Baada ya Herode kufariki familia ikarudi Jerusalemu lakini kwa vile mtoto wa Herode alikuwa akitawala pale, familia ikabakia Galilaya. Hivyo, sehemu kubwa ya maisha ya Kristo yalikuwa ni Galilaya lakini yeye alikuwa nabii aliyezaliwa Jerusalemu.
SALA: Ee Mungu tujalie kuyashika yaliyo sahihi na uyafungue masikio ya moyo wangu ili nisikilize maneno ya manabii wako na kuyashika.