Aprili 1,2022; Ijumaa: Juma la 4 la Kwaresma

Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Hek. 2: 1, 12-22

Wasiomsadikia Mungu walisema hivi, huku wakifikiri yasiyo kweli, “Zaidi ya hayo na tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu; atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu. Asema ya kwamba anamjua Mungu, na kujiita mtumishi wa Bwana. Ametuwia magombezi ya fikra zetu. Hata kumtazama twaona ni kugumu; maana maisha yake si sawasawa na maisha ya wengine, na mwenendo wake ni wa kigeni. Tunahesabiwa naye kuwa kama madini hafifu; anajitenga na njia zetu kama na uchafu. Wenye haki wasema kuwa mwisho wao ni heri; hujivuna ya kwamba Mungu ndiye baba yake. Haya na tuone kama maneno yake ni kweli; tufanye kujaribu yatakayompata wakati wa mwisho wake; mradi mwenye haki akiwa ni mwana wa Mungu, Yeye atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawasawa na maneno yake.” Ndivyo walivyosemezana, wakakosea kabisa. Kwa maana uovu wao uliwapofusha; hawakuzijua siri za Mungu; wala hawakuutarajia mshahara wa utakatifu, wala kudhani ya kwamba iko thawabu kwao wenye roho zisizo na hatia.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 34:16-20, 22

  1. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
    Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
    Walilia, naye Bwana akasikia,
    Akawaponya na taabu zao zote.

K: Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo.

  1. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
    Na waliopondeka roho huwaokoa.
    Mateso ya mwenye haki ni mengi,
    Lakini Bwana humponya nayo yote. (K)
  2. Huihifadhi mifupa yake yote,
    Haukuvunjika hata mmoja.
    Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
    Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)

INJILI: Yn. 7: 1-2, 10, 25-30

Wakati ule, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya; maana hakutaka kutembea katika Uyahudi, kwa sababu Wayahudi walikuwa wakitafuta kumwua. Na sikukuu ya Wayahudi, Sikukuu ya vibanda, ilikuwa karibu. Hata ndugu zake walipokwisha kukwea kuiendea sikukuu, ndipo yeye naye alipokwea, si kwa wazi bali kana kwamba kwa siri. Basi baadhi ya watu wa Yerusalemu wakasema, “Je! Huyu siye wanayemtafuta ili wamwue? Na kumbe! Anena waziwazi, wala hawamwambii neno! Yamkini hao wakuu wanajua hakika ya kuwa huyu ndiye Kristo? Lakini huyu twamjua atokako; bali Kristo atakapokuja hakuna ajuaye atokako.” Basi Yesu akapaza sauti yake hekaluni, akifundisha na kusema, “Mimi mnanijua, na huko nitokako mnakujua; wala sikuja kwa nafsi yangu; ila yeye aliyenipeleka ni wa kweli, msiyemjua ninyi. Mimi namjua, kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma.” Basi wakatafuta kumkamata; lakini hakuna mtu aliyeunyosha mkono wake ili kumshika, kwa sababu saa yake ilikuwa haijaja bado.

TAFAKARI
SAA YAKE BADO: Katika Injili ya leo tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo, akiwa amejongea kwa sherehe za Pasaka katika mji wa Yerusalemu. Na Wayahudi walizoea kumwona Kristo maeneo hayo na sasa wanaulizana, “Je, Pasaka hii atakuja au la?” Hawamwoni Kristo kwa vile hakuwa akionekana waziwazi kwa sababu tayari viongozi wa Wayahudi walikuwa wameshapanga kumkamata na kumuua. Lakini, Yesu alionekana tena akinena waziwazi ndipo watu walipoulizana kama kweli huyo ni Kristo. Bado wana shaka ya kumkubali Kristo. Wanajenga hoja ya kumkamata Kristo kwamba yeye sie. Ndipo Kristo anapaza sauti yake huku hekaluni akiwaambia yeye ndiye Kristo. Yeye anatoka kwa Mungu ambaye wao hawamjui, kwa maana wangemjua basi wangemwamini Kristo. Maneno hayo yanawafanya waone kwamba Kristo anawafananisha wao na watu wasiomjua Mungu, wanataka kumkamata. Lakini tunaambiwa hakuna mtu aliyenyoosha mkono wake kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado. Kristo mwenyewe alisema kwamba jambo lolote ambalo limeandikwa juu yake lazima litimie. Kristo alikuwa bado kukamilisha yote ambayo ametabiriwa.

SALA: Ee Mwenyezi Mungu, tunakushukuru kwa zawadi ya Kristo. Tunakuomba utuzidishie imani kuyaona yale yote ambayo ameyatenda, na kuamini kwamba yeye ndiye Kristo.