Machi 29,2022; Jumanne: Juma La 4 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Eze. 47: 1– 9, 12

Malaika alinileta mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupimia mkononi mwake, kwenda masharikini, akapima dhiraha elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viwiko vya miguu.

Kisha akapima dhiraha elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraha elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraha elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, “Mwanadamu, je! Umeona haya?” Kisha akanichukua, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, “Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko; maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 46:1-2, 4-5, 7-8

 1. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
  Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
  Kwa hiyo hayutaogopa ijapobadilika nchi,
  Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.

K: Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.

 1. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu,
  Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
  Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa;
  Mungu atausaidia asubuhi na mapema. (K)
 2. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
  Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
  Njoni myatazame matendo ya Bwana,
  Jinsi alivyofanya ukiwa katika mchi. (K)

INJILI: Yn. 5: 1-3, 5-16

Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza.

Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, “Wataka kuwa mzima?” Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu.” Yesu akamwambia, “Simama, jitwike godoro lako, uende.” Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, “Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro.” Akawajibu, “Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, ‘Jitwike godoro lako, uende.” Basi wakamwuliza, “Yule aliyekuambia, ‘Jitwike, uende, ni nani?’ Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, “Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya sabato.

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUTHAMINI VISAKRAMENTI: Visakramenti ni sala na Baraka ya Kanisa kwa watu na vitu. Moja ya visakramenti hivi ni maji ya Baraka. Maji yakibarikiwa tunayatumia kubarikia watu na vitu, na tunayatumia nyumbani katika sala na baraka. Zaidi sana, maji ya baraka yanawekwa mlangoni mwa kanisa na tunayatumia kwa sala ya toba tuingiapo kanisani. Kwa nini matumizi ya maji? Katika masomo ya leo tunapata ukweli kuwa maji yana nguvu ya uponyaji. Huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo palikuwa na birika, liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha. Katika birika hilo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wakienda kupata uponyaji. Maji bado yana nguvu ya uponyaji. Mama kanisa ametuwekea maji ya Baraka yenye nguvu ya uponyaji na ulinzi. Tunapoyatumia vilivyo, yana nguvu ya kutuondolea dhambi ndogo. Pia maji ya Baraka yanatuletea ulinzi dhidi ya ibilisi. Mt. Teresea wa Avila anatufundisha kuwa yeyote anayepiga ishara ya msalaba kwa kutumia maji ya Baraka anajiweka mbali kabisa na ibilisi. Wakatoliki tuache kudharau visakramenti na nguvu zake na tufahamu kuwa wenzetu wa madhehebu mengine wanatambua nguvu zilizomo na wanavitumia visakramenti kwa wingi.

SALA: Ee Bwana, asante kwa zawadi ya baraka na ulinzi wako kupitia visakramenti. Utujalie heshima na matumizi mazuri ya visakramenti hivyo. Amina.