Machi 28, 2022; Jumatatu: Juma La 4 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Isa. 65:17-21

Bwana asema: “Tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha. Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza. Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 30:1, 3-5, 10-12

 1. Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
  Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
  Umeniinua nafsi yangu,
  Ee Bwana, kutoka kuzimu.
  Umenihuisha na kunitoa
  Miongoni mwao washukao shimoni.

K: Nitakutukuza, ee Bwana, kwa maana umeniinua.

 1. Mwimbieni Bwana zaburi,
  Enyi watauwa wake.
  Na kufanya shukrani.
  Na kumbukumbu la utakatifu wake.
  Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
  Katika radhi yake mna uhai.
  Huenda kilio huja kukaa usiku,
  Lakini asubuhi huwa furaha. (K)
 2. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
  Bwana, uwe msaidizi wangu.
  Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
  Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
  Ee Bwana, Mungu wangu,
  Nitakushukuru milele. (K)

INJILI: Yn. 4:43-54

Wakati ule, Yesu aliondoka Samaria, akaenda Galilaya. Kwa maana Yesu mwenyewe alishuhudia ya kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe. Basi alipofika Galilaya, Wagalilaya walimpokea; kwa kuwa wameyaona mambo yote aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu; maana hao nao waliiendea sikukuu. Basi alifika tena Kana ya Galilaya, hapo alipoyafanya yale maji kuwa divai. Na palikuwa na diwani mmoja ambaye mwanawe hawezi huko Kapernaumu. Huyo aliposikia ya kwamba Yesu amekuja kutoka Uyahudi mpaka Galilaya, alimwendea, akamsihi ashuke na kumponya mwanawe; Kwa maana alikuwa kufani. Basi Yesu akamwambia, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?” Yule diwani akamwambia, “Bwana, ushuke asijakufa mtoto wangu.” Yesu akamwambia, “Enenda; mwanao yu hai.” Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye akashika njia. Hata alipokuwa akishuka, watumwa wake walimlaki, wakisema ya kwamba mtoto wake yu hai. Basi akawauliza habari ya saa alipoanza kuwa hajambo; nao wakamwambia, “Jana, saa saba, homa ilimwacha.” Basi babaye akafahamu ya kuwa ni saa ile ile alipoambiwa na Yesu, ‘Mwanao yu hai.’ Akaamini yeye na wote wa nyumbani mwake. Hiyo ni ishara ya pili aliyoifanya Yesu, alipokuwa ametoka Uyahudi kufika Galilaya.

TAFAKARI
KWARESMA NI KIPINDI CHA KUKOLEZA IMANI: Leo tunamuona Yesu akienda Galilaya, alikokulia. Anajiandaa kwa Sikukuu ya Pasaka. Lakini, kulikuwepo na Diwani mmoja aliyegundua kuwa Yesu yupo. Naye, alienda kumweleza Kristo yaliyompata. Mwanawe ambaye alikuwa mgonjwa mno karibu kufa. Alimwomba Kristo amponye mwanawe. Kristo anajaribu kumpima imani yake lakini yule Diwani anaona ni kama anamchelewesha. Anakuwa na imani thabiti kiasi cha kumwambia Kristu afanye haraka isije mwanawe akafa. Kristu anaiona imani hiyo na anaamua kumponya mwanawe, kwa kuongea tu. Anamwambia yule Diwani aende na mwanawe atapona. Anaamini neno la Kristo na anarudi kwake. Ndipo njiani anakutana na watu wake na anaambiwa kwamba amepona. Imani inatupa mwanga, inafungua milango ya elimu katika maisha. Unapokuwa na imani, tunakuwa na uhakika wa kufanikiwa katika mambo mengi sana. Tukitaka kufanikiwa, tuwe na imani. Lakini tukitaka tu kuwa na shaka ya maisha, basi tupoteze imani. Kipindi hiki cha Kwaresma tukitumie vizuri kuendelea kukoleza imani. Imani ambayo itatupa mwanga katika maisha.

SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristu tunakuomba utuongezee imani.