Machi 27,2022; Jumapili: Jumapili Ya 4 Ya Mwaka.

SOMO 1: Yos. 5: 9a, 10-12

Bwana akamwambia Yoshua, “Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi ya nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo. Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 34:1-6

 1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
  Sifa zake kinywani mwangu daima.
  Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
  Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

K: Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

 1. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
  Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
  Nalimtafuta Bwana akanijibu’
  Akaniponya na hofu zangu zote.
 2. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
  Wala nyuso zao hazitaona haya.
  Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
  Akamwokoa na taabu zake zote

SOMO 2: 2Kor. 5: 17-21

Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita; tazama! Yamekuwa mapya. Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika yeye.

SHANGILIO Lk.15:18

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia,
Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.

INJILI: Lk. 15: 1-3, 11-32

Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.” Akawaambia mfano huu, akisema. “Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, ‘Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia.”’ Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, “Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, ‘Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.’”Akaondoka, akaenda kwa babaye.

Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana akamwambia, “Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.” Lakini baba aliwaambia watumwa wake, “Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteeni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.” Wakaanza kushangilia.

Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, “Mambo haya, maana yake nini?” Akamwambia, “Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.” Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, “Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.” Akamwambia, “Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”

TAFAKARI
TUAMUE KWA DHATI KUACHA DHAMBI: Wazo hili linatoka katika Injili yetu na linaungwa mkono na masomo yanayoisindikiza. Wayahudi walikuwa wamejigawanya wenyewe katika makundi mawili: kundi la waendao mbinguni na kundi la waendao motoni. Kundi la waendao mbinguni lilihusisha Mafarisayo, waandishi wa sheria, makuhani na wakuu wa makuhani, Waeseni na Wazeloti. Kwa upande mwingine, wale waendao motoni, “piga ua”, ndio waitwao katika Injili zetu “wenye dhambi”, walitiwa watoza ushuru wote, makahaba wote, washona viatu wote na wachunga wanyama wote.
Mgawanyo huu uliochagizwa na Mafarisayo (marabi) ulitokana na kigezo cha mtu kuwa na muda wa kuishughulikia torati. Walisema mtu akiwa na muda kuishughulikia torati atajua Mungu anataka nini. Mtu akijua Mungu anataka nini atafanya. Mtu akifanya anachotaka Mungu, Mungu atamkaribisha mbinguni.
Kinyume chake, mtu asipokuwa na muda kuishughulikia torati hatajua Mungu anataka nini. Mtu asipojua Mungu anataka nini hatafanya. Na mtu asipofanya anachotaka Mungu, Mungu atamtupa motoni. Ni kwa namna hii katika kundi la waendao mbinguni wakajiweka Mafarisayo wenyewe, waandishi wa sheria, makuhani na wakuu wa makuhani, Waeseni na Wazeloti. Kwa upande mwingine, wakawaweka waendao ndio “wadhambi” au “wenye dhambi”, walitiwa watoza ushuru wote, makahaba wote, washona viatu wote na wachunga wanyama wote. Watu wa makundi haya mawili hawakutarajiwa kuchangamana.
Yesu alipofika alitiwa na wale waendao mbinguni katika kundi lao na hivyo hawakutarajia kuonekana wakichangamana na wadhambi. Jambo hili ndilo analolijibu kwa namna mbalimbali. Leo katika Injili ya Luka aliwajibu kwa mifano mitatu mizuri. Wadhambi ni kama kondoo mmoja aliyepotea, Mungu anafanya kila juhudi kuwatafuta na wakipatikana anafurahi sana. Halafu wadhambi ni kama shilingi iliyopotea kati ya kumi, Mungu anafanya kila awezalo kuwatafuta na wakipatikana anafurahi sana. Na hatimaye ndiyo mfano huu uliosomwa. Wadhambi ni kama mwana mpotevu, wakiamua kwa dhati kuacha dhambi na kurudi, Mungu anawapokea kwa furaha na kuwarejeshea hadhi yao ya kuwa wana.
Mwana mpotevu alifanya mambo ya kikatili. Alijirithisha mali kabla baba yake hajafa. Halafu aliyaponda mali na makahaba katika nchi ya mbali. “Alijichana”. Alijilisha pamoja na makahaba. Kufilisika na njaa vilimtia adabu. Basi, kwa kuyasoma mazingira yake ya dhiki, alizingatia moyoni mwake, akajutia utundu wake, akaamua kurudi kwa baba na kumwomba msamaha. Naye baba alimsamehe mwanawe huku akimrejeshea nafasi yake ya kuwa mwana kwa gharama ya karamu nono. Kumbe ndiyo hapa tunapoalikana tuhusike. Mungu ni mwenye huruma sisi tuamue kujipatanisha naye.
Somo la kwanza linatangaza jinsi Mungu alivyo mwema, jinsi anavyoachilia kwa msamaha utovu na dhambi za watu. Somo la pili linatangaza kwamba kila mtu anakuwa mpya katika Kristo. Kazi inabaki kwake kushikamana, maana Kristo kwa ajili yetu wadhambi, yupo tayari kuchukuliana nasi hadi tuupate uzima wa milele.
Hii ni Habari Njema kweli kweli. Tusifanye masihara wala uzembe; tutumie muda huu kuamua kuachana na dhambi zetu tujipatanishe salama na Mungu wetu.

SALA: Ee Yesu Kristo, tutambulishe jinsi ulivyokuja kwa ajili yetu sisi wadhambi. Tushujaishe, tuzingatie mioyoni mwetu, turudi kwa Baba yetu mwema. Amina.