Machi 26,2022;Jumamosi: Juma La 3 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Hos. 5:15-6:6

Bwana asema: “Katika taabu yao watanitafuta kwa bidii: Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. Ee Efrahimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo, nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:1-2, 16-19

 1. Ee Mungu, unirehemu,
  Sawasawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.
  Unioshe kabisa na uovu wangu,
  Unitakase dhambi zangu.

K: Ninavyotaka ni fadhili, si sadaka.

 1. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
  Moyo uliovunjika na kupondeka,
  Ee Mungu, hutaudharau. (K)
 2. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
  Uzijenge kuta za Yerusalemu.
  Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki,
  Na sadaka za kuteketezwa, na kafara (K)

INJILI: Lk. 18:9-14

Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. “Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru.” Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang`anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.” Lakini yule mtoza ushuru alisisima mbali, wala hakudhubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema,” Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.” Nawaambia, “Huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhilie atakwezwa.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA TOBA: Katika somo la Injili Bwana wetu Yesu Kristo anatupatia mfano wa watu wawili waliopanda hekaluni kusali. Mmoja ni Farisayo na mwingine ni mtoza ushuru. Wote walienda kusali lakini ni mmoja tu aliyeweza kufaidika, naye ni mtoza ushuru. Farisayo hakufaidika kwa vile alijivunia matendo yake. Ndio tunaalikwa daima kutenda mema, lakini hatuhitaji kusifiwa kwa hayo mpaka kuyaleta katika sala. Kinyume chake, mtoza ushuru anajitambua kuwa mbele ya Mungu yeye ni mdhambi na hivyo anaomba toba. Tunaambiwa yeye alihesabiwa haki kuliko Farisayo. Kumbe, suala si kupata kwenda kanisani tu kusali, la muhimu ni kufaidika na huko kwenda kanisani. Tusiende kanisani kwa mazoea kiasi kwamba huoni tofauti kabla na baada ya kutoka kanisani. Ili kufaidika na nyakati za sala tunahitaji kwanza kabisa kuwa na maandalizi. Tuwe na nia na malengo ya sala hiyo. Tusiwakwaze wengine wakati wa sala. Wakati wa sala tuishushe mioyo yetu kwake Mungu na tumuombe atushibishe kwa fadhili zake. Tutumie vizuri kwaresima hii kusali kwa toba.

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, nijalie moyo mkunyufu wakati was ala ili niweze kuchota Baraka na neema zako kwa njia ya sala.