Kupashwa Habari Ya Kuzaliwa Bwana
Sherehe
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Isa 7: 10-14
Bwana alisema na Ahazi akinena, “Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana.” lakini Ahazi akasema, “Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana.” Naye akasema, “Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu Pia?” Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Wimbo Wa Katikati Zab.40:6-10
- Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
K: Tazama, nimekuja, Ee Bwana,
kuyafanya mapenzi yako.
- Katika gombo la chuo nimeandikiwa54
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sharia yako imo moyoni mwangu. (K) - Nimehubiri habari za haki katika kusanyika kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K) - Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyikko kubwa. (K)
SOMO 2: Ebr. 10:4-10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, “Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi, hukupendezwa nazo.” Ndipo niliposema, “Tazama, nimekuja, (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.” Hapo juu asemapo: Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo, (Zitolewazo kama ilivyoamuru torati), Ndipo aliposema: Tazama nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.
INJILI: Lk. 1:26-38
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, “Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe.” Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, “Salamu hii ni ya namna gani?” Malaika akamwambia, “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.” Mariamu akamwambia malaika, “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?” Malaika akajibu akamwambia, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.” Mariamu akasema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
TAFAKARI
MRADI MKUBWA WA UKOMBOZI UNAANZA KWA AJILI YETU: Leo tunangaziwa jinsi Mungu alivyotuanzishia mradi mkubwa wa ukombozi wetu. Dhambi ya Adamu na Eva iliuzamisha upendo wa Mungu na mwanadamu akamwaga mboga yao. Kufuatia utovu huo wa utii, Mungu hakujibu kwa hasira. Badala yake Mungu aliahidi kutukomboa kwa njia ya mzaliwa wa mwanamke (Mwa 3:15). Mungu halipi uovu kwa uovu. Alimuumba mwanadamu kwa upendo akaamua kuendeleza upendo. Kwa kuwa (Mwa 3:15) humtaja mwanamke atakayemzaa mtoto mwanaume atakayemponda kichwa Shetani na kwa namna hiyo kumdokeza Bikira Maria atakayemzaa Yesu Masiya atakayemshinda Shetani, aya hiyo huitwa kwa haki “injili ya mwanzo”, kwa Kilatini “protoevangelium”.
Kumbe, sherehe ya leo ndiyo kuanza kutekelezwa kwa ahadi ya kale. Wanadamu walipaswa kumsubiri Masiya kwa miaka mingi kadiri alivyoamua Mungu mwenyewe. Kifupi, kupashwa habari Bikira Maria ndiyo mwanzo wa kutekelezwa kwa ahadi ya wanadamu kupatiwa Masiya. Na kwa kadiri ya hesabu za Wayahudi hadi Yesu anazaliwa ilipita miaka 4000.
Wapo wanadamu waliodhani Mungu aliwatania au aliwadanganya wanadamu. Kumbe, leo basi anamtuma mjumbe wake, malaika Gabrieli kumtangazia mwanamwali aliyeteuliwa rasmi awe mhusika muhimu katika mradi wa kuzaliwa Yesu Kristo. Kwa haya anayotukiza Mungu leo, anajipambanua mwenyewe kama Mungu mwenye upendo kwa viumbe vyake na mwaminifu kwa ahadi zake. Miaka 4000 kwa Mungu haikuwa mingi kwani hesabu za muda kwa yeye aliye wa milele ni tofauti na zetu sisi wenye maisha yenye kikomo. Tunaambiwa siku zote kwamba kwa Mungu miaka elfu ni kama siku moja na siku moja kama miaka elfu (Zab 90:4, 1 Pet 3:8).
Somo la kwanza linadokeza hali ilivyokuwa katika Israeli watu walipokuwa wameduwazwa na kile walichodhani Mungu kutokutelekeza ahadi ya kuwaletea wanadamu Masiya. Wengine walitambua methali ya, “Subira yavuta heri”. Ahazi ni mmoja wao. Vyovyote vile ilivyokuwa, Mungu alijua shauri lile lilikuwa ni lake mwenyewe ikawa ananuia kuwapa ishara ya ajabu. Kudhihirishwa kwa ishara hiyo ndiyo sherehe yetu ya leo: bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
Somo la pili ndilo linalotupa maana ya kiroho ya ishara husika. Yesu Kristo, neno la Mungu anatwaa mwili (anajimwilisha) kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria kusudi apate damu na mwili atakavyotolea sadaka azizi, sadaka itakayopikua sadaka zote dhalili, za wanyama na nafaka ambazo wanadamu walikuwa wakitolea katika kujaribu kujipatanisha na Mungu.
Tukijumlisha, kumbe sherehe ya leo ni mwanzo wa mradi wa kikarimu wa kutukomboa tuliokoroga mambo. Kwa namna hii, hii ni sherehe ya kusherehekewa kwa vifijo, shangwe na shukrani kwa Mungu mwema ambaye uaminifu wake kwa ahadi zake hauna kasoro yoyote.
SALA: Ee Mungu tunakushukuru kwa kutuumba na kutuanzishia mwenyewe mradi wa kutokomboa. Dhambi ya Adamu na Eva iliharibu uhusiano wetu. Kumbe, unamleta Mwanao aturekebishie uhusiano wetu nawe. Tunakushukuru. Amina.