SOMO 1: Yer. 7:23-28
Naliwaamuru neno hili, nikisema, “Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru, mpate kufanikiwa. Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele. Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma. Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao.” Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza; nawe utawaita; lakini hawatakuitikia. Nawe utawaambia, “Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao.”
Wimbo Wa Katikati Zab. 95:1-2, 6-9
- Njoni, tumwimbie Bwana,
Tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.
Tuje mbele zake kwa shukrani,
Tumfanyie shangwe kwa zaburi.
(K) Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu.
- Njoni, tuabudu, tusujudu,
Tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba.
Kwa maana ndiye Mungu wetu,
Na sisi tu watu wa malisho yake,
Na kondoo za mkono wake. (K) - Ingekuwa heri leo msikie sauti yake!
Msifanye migumu mioyo yenu;
Kama vile huko Meriba,
Kama siku ya Masa jangwani.
Hapo waliponijaribu baba zenu,
Wakanipima, wakayaona matendo yangu. (K)
INJILI: Lk. 11: 14-23
Yesu alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu. Wengine wao wakasema, “Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Wengine walimjaribu, wakitaka ishara itokayo mbinguni. Naye akajua mawazo yao, akawaambia, “Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka. Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli. Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu. Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia. Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama; lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang’anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake. Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutapanya.”’
TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUKUBALI MAFANIKIO YA WENGINE: Sisi binadamu tunakuwa wagumu sana wakati fulani kukubali na kuona mafanikio ya wengine. Tunashindwa kuona ukweli kuwa wenzetu wanaweza kufanya makubwa kutokana na jitihada zao na upendeleo toka kwa Mwenyezi. Tunapoona mafanikio ya wenzetu basi tunaona pengine wamebahatisha tu au labda wametumia njia mbadala kufikia mafanikio hayo. Katika somo la injili tunamuona Bwana wetu Yesu Kristo akimtoa mtu pepo bubu. Pepo anapotoka mtu huyo anaanza kuzungumza. Watu wenye hila wanapoona hilo, badala ya kumshukuru Mungu kwa uponyaji huo wao wanajenga hoja kuwa Kristo ametoa pepo kwa Beelzebuli. Wanatafuta sababu za mbali za kufifisha uwezo wa Mwenyezi Mungu kupitia mwanawe Yesu Kristo. Ndivyo nasi tunavyofanya katika maisha yetu ya kila siku. Hatuoni jitihada na upendeleo we Mungu katika mafanikio ya wenzetu. Kipindi hiki cha Kwaresima kitusaidie kutambua kuwa Mungu bado anafanya kazi kupitia kwa wenzetu.
SALA: Ee Mungu unijalie niuone uwezo wako kupitia mafanikio ya wenzangu.