Machi 23,2022; Jumatano: Juma La 3 La Kwaresima

Toribio wa Mogrovejo, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Kum. 4: 1, 5-9

Musa aliwaambia makutano: “Ee Israeli, zisikilizeni amri na hukumu niwafundishazo, ili mzitende; mpate kuishi na kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wa baba zenu. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama Bwana, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, ‘Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama Bwana, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo? Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako.’”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 147:12-13, 15-16, 19-20

  1. Msifu Bwana, Ee Yerusalemu;
    Msifu Mungu wako, Ee Sayuni.
    Maana ameyakaza mapigo ya malango yako,
    Amewabariki wanao ndani yako.

K: Msifu Bwana, Ee Yerusalemu.

  1. Huipeleka amri yake juu ya nchi,
    Neno lake lapiga mbio sana.
    Ndiye atoaye theluji kama sufu,
    Huimwaga barafu yake kama majivu. (K)
  2. Humhubiri Yakobo neno lake,
    Na Israeli amri zake na hukumu zake.
    Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo,
    Wala hukumu zake hawakuzijua. (K)

INJILI: Mt. 5: 17-19
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.” Kwa maana, amin, nawaambia, “Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie. Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUSHIKA AMRI: Kila taasisi lazima iwe na miongozo itakayoisaidia iweze kujiendeleza kwa utaratibu. Vyama na vikundi daima huwa na katiba ambayo inaratibisha maisha ya kila siku ya umoja. Nasi katika imani sharti tuwe na mwongozo. Hivyo, Mwenyezi Mungu ametuwekea amri ambazo ni mwongozo wa nini cha kufanya na nini cha kuacha ili kuleta amani na uelewana katika jamii. Amri hizo ni njia zinazotusaidia kufika kule tulipopanga kufika. Katika Injili Kristo, anasema kuwa yeye amekuja kutimiliza torati na manabii na siyo kuzitengua. Anakuja kutoa tafsiri sahihi ya hizo sheria ili kutusaidia kuzifuata kwa ukamilifu. Anasisitiza kuwa mbingu na nchi zitapita ila sheria hizo hazitadondoka hata nukta moja. Mwisho anatuhimiza kuzishika na kufundisha wengine ili kustahili kuwa wakubwa katika ufalme wa mbinguni. Anatuonya kuwa kutozishika na kuzifundisha basi tutakuwa wadogo katika Ufalme wa Mbinguni. Nani hapendi kuwa mkubwa mbinguni? Hebu tuzishike amri na kuzifundisha kwa vitendo kwa wenzetu. Kwaresima hii itupe mazoezi mazuri ya kufuata amri za Mungu.

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi nijalie uchaji wako. Nizipende amri zako na kuzitenda.