Machi 22, 2022; Jumanne: Juma La 3 La Kwaresima

Urujuani Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Dan. 3: 25, 34-43

Ndipo Azaria akasimama akasali hivi, akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema: “Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako, wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa ajili ya Ibrahimu umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu wako, ambao uliwaahidia ya kuwa utauzidisha uzao wao kama nyota za mbinguni na kama mchanga uliopo pwani. Maana sisi, Ee Bwana, tumekuwa duni kuliko mataifa mengine yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema. Lakini kwa moyo uliovunjika na roho nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika. Na sasa tunakufuata kwa moyo wote; tunakucha, na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawa sawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 25:4-9

 1. Ee Bwana unijulishe njia yako,
  Unifundishe mapito yako,
  Uniongoze katika kweli yako,
  Na kunifundisha.

K “Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.”

 1. Ee Bwana kumbuka rehema zako na fadhili zako,
  Maana zimekuwako tokea zamani.
  Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
  Wala maasi yangu.
  Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)
 2. Bwana yu mwema, mwenye adili,
  Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
  Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
  Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)

INJILI: Mt. 18: 21-35

Petro alimwendea Yesu akamwambia, “Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? hata mara saba?” Yesu akamwambia, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyonavyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, ‘Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.’” Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.

Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, “Nilipe uwiwacho.” Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, “Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.” Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni.

Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe je! haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUSAMEHE SANA: Bwana wetu Yesu Kristo anatoa mfano wa mtu anayesamehewa lakini yeye anakuwa mgumu kusamehe. Kristo anatufundisha kwa nini tunapaswa kusamehe wenzetu, naye anatoa sababu mbili. Kwanza msamaha ni kigezo cha sisi pia kusamehewa. Tunafundishwa katika heri nane kuwa, “Heri wenye rehema, maana hao watapata rehema”. Pia tunasali katika sala ya Bwana tukiomba atusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe walio tukosea. Hivyo msamaha ni kigezo cha sisi pia kusamehewa. La pili ni kuwa kile wenzetu wanatukosea ni kidogo sana ukilinganisha na kile ambacho sisi tunamkosea mwenyezi Mungu.
Lakini Mungu anatusamehe. Katika mfano wa mdeni anayedaiwa na kusamehewa talanta elfu kumi anashindwa naye mwenziwe deni dogo la dinari mia moja. Taarifa zinapomfikia wake anaghadhibika na kumtia hukumuni. Kristo anahitimisha kuwa tusipowasamehe wenzetu pia sisi hatutasamehewa. Baba anakavyotutenda sisi tusipowasamehe kwa mioyo yetu ndugu zetu wanaotukosea. Katika kipindi hiki cha kwaresema tuvune moyo wa msahama.

SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristo unijalie moyo wa msamaha, niwe mwepesi kusamehe na kusahau.