Machi 20, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 3 Ya Mwaka

SOMO 1: Kut. 3: 1-8a, 13-15

Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, Kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, “Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei.” Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, “Musa! Musa!” Akasema, “Mimi hapa.” Naye akasema, “Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.” Tena akasema, “Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo.” Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu.

Bwana akasema, “Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali.” Musa akamwambia Mungu, “Tazama, nitakapofika kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, ‘Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, jina lake n’nani? Niwaambie nini?”’ Mungu akamwambia Musa, “Mimi niko ambaye niko,” akasema, “Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli; Mimi niko amenituma kwenu.” Tena Mungu akamwambia Musa, “Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 103:1-4, 6-8, 11

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
  Naam, vyote vilivyo ndani yangu
  Vilihimidi jina lake takatifu.
  Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

 1. Akusamehe maovu yako yote,
  Akuponya magonjwa yako yote,
  Aukomboa uhai wako na kaburi,
  Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
 2. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
  Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
  Alimjulisha Musa njia zake,
  Wana wa Israeli matendo yake. (K)
 3. Bwana amejaa huruma na neema,
  Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
  Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
  Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)

SOMO 2: 1 Kor. 10: 1-6, 10-12

Ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msinung’unike, kama wengine wao walivyonung’unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.

SHANGILIO Zab. 95:8
Msifanye migumu mioyo yenu;
Lakini msikie sauti yake Bwana.

INJILI: Lk. 13: 1-9

Wakati ule walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, “Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo?” Nawaambia, “Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu?” Nawaambia, “Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” Akanena mfano huu, “Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate.” Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, “Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?” Akajibu akamwambia, “Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.”

TAFAKARI
TUKITUBU, MUNGU ANATUHURUMIA NA KUTUONDOLEA HOFU: Wazo hili linapatikana katika Injili, nalo linaungwa mkono na masomo mengine yaliyosomwa leo. Wayahudi kama wanadamu wengine tulivyo walipenda sana kutafuta mbona watu wapatwe na madhila makubwa. Kinyume na tulivyozoea sisi watu weusi kuelezea mikasa inayowafika watu kwa kusema kuna “mkono wa mtu” yaani ulozi, wao walisema kuna “mkono wa Mungu”, yaani adhabu kutoka kwa Mungu mwenyezi kufuatia dhambi fulani aliyoitenda anayeteseka.
Hivyo Wayahudi wanaofika kumsimulia Yesu Wasamaria kadhaa walivyouawa na Pilato licha ya kwamba walikuwa wakifanya ibada karibu wanako jibu lao la kwamba walitenda dhambi fulani. Yesu alitambua mawazo yao ndipo akawaambia wasiwashwe na mkasa wa Wasamaria. Papo hapo akawaongezea mkasa wa Wayahudi wa Yerusalemu walioporomokewa na mnara. Akawaambia iwe kwa sababu ya dhambi au kwa sababu nyingine yoyote si shauri muhimu, muhimu ni watu wote kutubu, la sivyo wataangamia pia. Ndipo hapo hapo akawapigia mfano wa mtini usiozaa uliokuwa unaiharibu ardhi bure uliombewa huruma ya kutazamiwa kama ukipaliliwa na kutiliwa samadi utazaa au la. Aliyeuombea radhi alisema mti huo usipozaa baada ya kufanyiwa vyema hivyo, itakuwa halali kuukatilia mbali. Kifupi kwa maelezo na mfano huo, Yesu alitaka kuwaambia walimwengu, watubu kwani kuendelea kwao kuishi hapa duniani si kwa sababu wanaogopwa na Mungu isipokuwa wanahurumiwa tu.
Somo la kwanza liko katika mstari huu huu. Musa anaitwa akawakomboe Waisraeli waliokuwa wakitumikishwa huko Misri. Mungu amewahurumia tu si kwamba wamekuwa waadilifu sana. Mungu atawakomboa na kuwapa nafasi ya kutazamiwa watakavyoendana na wema wa kukombolewa waliotendewa bure. Kilichoendelea twakijua. Waisraeli waliendeleza utundu hata Mungu akawaruhusu wapelekwe uhamishoni Babiloni (mwaka 587 K.K). Walilitafuta, wakalipata!
Somo la pili liko wazi kabisa katika wazo la wanadamu kuombwa tutubu kwani tunahurumiwa na Mungu tu wala hatuogopi. Waisraeli ambao walipata namna ya ubatizo kwa kuongozwa na nguzo ya moto jangwani, kisha wakalishwa manna kunyweshwa maji jangwani, hawakujifunza kutulia badala yake waliendekeza utukutu na manung’uniko hata Mungu akaruhusu wafie jangwani wala wasionje raha za nchi ya ahadi. Somo linasema hayo yaliwafika ili sisi tupate mfano na tujitambue.
Nadhani hakuna namna nyingine bora zaidi ya kueleza hitaji la kutubu na kuachana na maisha yetu dhambi, ila kutubu. Tukifanya hivyo, Mungu Mwenyezi anatuhurumia na kutuondolea hofu. Tulio wengi tupo kama mtini uliombewa radhi na mtunzaji bustani tu ili usifanyiwe haraka ya kukatwa bali upewe nafasi ya kupaliliwa na kutiliwa samadi na ikiwa huduma hizo hazitafua dafu ndipo ukatiliwe mbali. Sisi ndiyo mitini. Yesu Kristo ndiye mtunza bustani. Kupaliliwa ndiko huku kutunzwa na kupewa afya na Mungu, kutiliwa mbolea ndiko huko kulishwa Ekaristi Takatifu (Mwili na Damu ya Yesu Kristo). Kama mwaka huu, ndiyo muda huu tunaopewa kuishi hapa duniani, hatutazaa chochote, Mungu atatukatilia mbali, yaani atatutupa jehanamu. Haya shime tuikamate rehema hii, tusimtie Mungu vidole puani. Kumbe, tutangaziane toba kwani muda ndio huu kabla hatujaharibikiwa.

SALA: Ee Mungu mwema, tunakushukuru kwa kutuhudumia huku ukitusubiri tuzae matunda. Tafadhali ongeza dhati yetu ya kushirikiana nawe ili tuzae matunda ya wema unayotutazamia tuzae. Usitukate mapema, tujirekebishe. Amina.