Machi 18, 2022; Ijumaa: Juma La 2 La Kwaresima

Mt. Sirili wa Yerusalemu, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO I: Mwa. 37:3-4, 12-13, 17-28

Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu. Israeli akamwambia Yusufu, “Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo nikutume kwao.” Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani. Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue. Wakasemezana wao kwa wao, “Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, ‘Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.’” Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue. Reubeni akawaambia, “Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake.” Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa, wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji. Nao wakakaa kitako kula chakula. Wakainua macho yao, wakaona msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri. Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake? Haya na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yenu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali. Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 105:16-21

 1. Akaiita njaa iijilie nchi,
  Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.
  Alimpeleka mtu mbele yao,
  Yusufu aliuzwa utumwani.

K: Zikumbukeni ajabu zake Bwana alizozifanya.

 1. Walimwumiza miguu yake kwa pingu,
  Akatiwa katika minyororo ya chuma.
  Hata wakati wa kuwadia neno lake,
  Ahadi ya Bwana ilimjaribu. (K)
 2. Mfalme alituma watu akamfungua
  Mkuu wa watu akamwachia.
  Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,
  Na mwenye amri juu ya mali zake zote. (K)

INJILI: Mt. 21: 33-43; 45-46

Yesu aliwaambia wakuu wa makuhani na wazee wa watu, “Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake. Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe. Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza, wakawatenda vile vile.”
Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, “Watamstahi mwanangu.” Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, “Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake.” Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua. Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima? Wakamwambia, “Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.” Yesu akawaambia, “Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu?” Kwa sababu hiyo nawaambia, “Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa, lingine lenye kuzaa matunda yake.” Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao. Nao walipotafuta kumkamata waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUZAA MATUNDA: Kristo anatoa mfano wa mtu aliyekuwa na shamba la mizabibu. Kwa jinsi alivyolipatia mahitaji muhimu, hakuwa na shaka juu ya kupata matunda. Wakati wa matunda ulipofika, aliwatuma matumwa wake kwa wakulima. Lakini watumwa hao hawakupata matunda na zaidi sana walitendewa vitendo vya kikatili na hata wengine kuuawa. Ndipo mwenye shamba alipomtuma mwanawe wa pekee akidhani ya kuwa wangemstahi. Lakini wakulima kwa tamaa ya kurithi mali, wakamuua. Kristo anauliza je, atakapokuja bwana wa shamba atawatenda nini hao wakulima? Wapendwa, dhambi inatia upofu. Ukiiendekeza dhambi unapoteza uwezo wa kuona jema lolote. Dhambi ina zaa dhambi na mwisho wake tunakuwa tayari kufanya lolote ili kuficha dhambi. Tukizoea sana dhambi tunakuwa watu wasio na huruma na hapo tunashindwa kuzaa matunda. Hapo maisha yetu hapa duniani yanakuwa si ya faida bali ya hasara. Kipindi cha Kwaresima tukitumie kwa kuchukia dhambi na hivyo kiwe kipindi cha kuzaa matunda. Maisha tumepewa kama dhamana.

SALA: Ee Mungu unijalie maisha yangu ya hapa duniani yawe ya faida kwa wengine, nizae matunda mema.