Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Yer. 18: 18-20
Waliposema, “Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yoyote. Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 31:4-5, 13-15
- Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
Mikononi mwako naiweka roho yangu;
Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
K “Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.”
- Maana nimesikia masingizio ya wengi;
Hofu ziko pande zote.
Waliposhauriana juu yangu,
Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K) - Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)
INJILI: Mt. 20: 17-28
Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, “Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeredi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.”
Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, “Wataka nini?” Akamwambia, “Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.” Yesu akajibu akasema, “Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi?” Wakamwambia, “Twaweza.” Akawaambia, “Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.”
Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, “Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.”
TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUWA MTUMISHI: Katika injili tunamuona mama wa wana wawili wa Zebedayo akimuomba Kristo awajalie watoto wake kuketi: mmoja mkono wa kuume na mwengine mkono wa kushoto katika ufalme wake. Kristo anawaambia kuwa hawajui waliombalo. Anawauliza kama wataweza kukinyea kikombe atakachonywea yeye. Wanamjibu kuwa wataweza. Anawatabiria kuwa kikombe watakinywea lakini kuhusu kuketi mkono wake wa kiume au kushoto ni suala la Mungu Baba kuamua. Na huo ndio ukweli kukinywea kikombe ni kupitia njia ya mateso. Yakobo alikuwa wa kwanza miongoni mwa Mitume kumwaga damu yake kwa ajili ya Kristo. Yohane yeye alikuwa wa mwisho miongoni mwa Mitume kufariki. Alifariki akiwa mzee lakini naye alionja kikombe cha Kristo hasa kwa kuishi uhamishoni katika visiwa vya Patmo. Ombi hili linasababisha mitume wengine wakasirikie. Ila Kristo anafundisha maana halisi ya ukubwa ambayo ni kutumika na kuwaonyesha wengine njia. Ukubwa ni kusimama badala ya wengine. Kila kiongozi aumize kichwa kuwasaidia watu anaowaongoza.
SALA: Ee Bwana wetu Yesu Kristo, uendelee kutujalia unyenyekevu, tukubali kutumikia katika madaraka yetu.