Machi 15,2022; Jumanne: Juma La 2 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Isa. 1: 10, 16-20

Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. “Haya, njoni, tusemezane,” asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 50:8-9, 16-17, 21-23

 1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
  Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
  Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
  Wala beberu katika mazizi yako.

K. Autengenezaye mwenendo wake,
Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.

 1. Una nini wewe luitangaza sheria yangu,
  Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
  Maana wewe umechukia maonyo,
  Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
 2. Ndivyo ulivyofanya, name nikanyamaza,
  Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe,
  Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza.
  Naye autegemeza mwenyendo wake,
  Nitamwonyesha wokovu na Mungu. (K)

INJILI: Mt. 23: 1-12

Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, “Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yoyote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUJINYENYEKESHA: Wanadamu tunapenda makuu. Pengine hili tumerithi katika ile dhambi ya asili. Maana wazazi wetu wa kwanza nao walidanganywa watakuwa kama Mungu na wakawa tayari kula tunda walilokatazwa. Katika injili Kristo anatuonyesha namna wanaopata madaraka wanajigeuza miungu watu. Wanawatwika wengine mizigo mizito. Tena hupenda sifa na heshima katika makusanyiko na kusalimiwa kwa kutajwa kwa vyeo vyao. Ukifanya hivyo utaelewana nao na utakula mema ya nchi. Kinyume chake utaonekana mpinzani. Kwa ubinadamu uliopitiliza wanajisahau sana na hata kuwaadabisha vikali watu wasiowapa sifa wanazohitaji. Kristo anatuhakikishia kuwa sifa ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na aliye Baba yetu na mwalimu na kiongozi wetu ni Kristo tu. Zaidi sana anatutaka kuwa waangalifu kwani huko kupenda kwetu kuwa wakuu kunaweza kutuletea anguko kubwa pale ambapo tutalazimika kushushwa. Kwaresima hii itunyenyekeshe sana hasa wale waliojaliwa madaraka.

SALA: Ee Mungu unijalie moyo wa unyenyekevu. Kadili unavyoniinua unijalie kunyenyekea zaidi.