Machi 14,2022; Jumatatu: Juma La 2 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 1
SOMO 1: Dan. 9: 4-10
Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki ina wewe lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 79:8-9, 11, 13

1.Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumeadhilika sana.

K: Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.

2.Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
Kwa ajili ya jina lako. (K)

3.Kuugua kwake aliyefungwa na kuingie mbele zako.
Kwa kadiri ya ya uweza wa mkono wako
Uwahifadhi wana wa mauti.
Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
Tutakushukuru milele;
Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

INJILI: Lk. 6:36-38
Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA HURUMA: Mwanadamu daima anapenda kuhurumiwa, kufarijiwa na hata kusaidiwa anapokuwa shidani. Je, kadiri ninavyopenda wengine wanitendee hivyo mimi nami nipo tayari kuwatendea wengine? Leo Kristo anatushauri tuwe watu wa huruma. Mungu wetu ni mwenye huruma na yupo tayari daima kutuhurumia na kutusamehe pale tunapomuendea kwa moyo wa toba. Tunapofaidi huruma hiyo ya Mungu, je, sisi huwafaidisha wengine kwa huruma yetu? Mtu anapotukosea tunapenda sana kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine. Muda fulani tunafurahia kuona makosa ya wenzetu na wanapokosea tunakosa muda wa kuongea nao. Huruma ni kujiweka katika nafasi ya mtenda kosa. Kufikiria, Je, kama ningekuwa mimi katika mazingira yale ningefanya nini? Pindi unapotambua kuwa hata wewe ungeweza kufanya vilevile ndio ujue kuwa huruma inatakiwa. Tusikimbilie kuhukumu maana tunaambiwa kipimo hichohicho tunachowapimia wengine ndicho tutakachopimiwa na sisi pia. Tuwe na huruma kama Baba yetu ili nasi tuhurumiwe.

SALA: Ee Mungu unijalie moyo wa huruma kwa wengine. Nishiriki taabu na maangaiko yao.