Machi 13, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 2 Ya Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mwa. 15: 5-12, 17-18

Mungu akamleta Ibrahimu nje, akasema, “Tazama sasa mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu.” Akamwambia, “Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.” Akamwamini Bwana, naye akamhesabia jambo hili kuwa haki. Kisha akamwambia, “Mimi ni Bwana, niliyekuleta kutoka Uru wa Wakaldayo nikupe nchi hii ili uirithi.” Akasema, “Ee Bwana Mungu, nipateje kujua ya kwamba nitairithi?” Akamwambia, “Unipatie ndama wa miaka mitatu, na mbuzi mke wa miaka mitatu, na kondoo mume wa miaka mitatu, na hua, na mwana njiwa.” Akampatia hao wote, akawapasua vipande viwili, akaweka kila kipande kuelekea mwenzake, ila ndege hakuwapasua. Hata tai walipotua juu ya mizoga Abramu akawafukuza. Na jua lilipokuwa likichwa usingizi mzito ulimshika Abramu, hofu ya giza kuu ikamwangukia. Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, “Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Frati.”

Wimbo Wa Katikati Zab. 27:1, 7-9, 13-14

  1. Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
    Nimwogope nani?
    Bwana ni ngome ya uzima wangu,
    Nimhofu nani?

(K) Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu.

  1. Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia,
    Unifadhili, unijibu.
    Moyo wangu umekuambia,
    Bwana, uso wako nitautafuta. (K)
  2. Usinifiche uso wako,
    Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
    Umekuwa msaada wangu, usinitupe,
    Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. (K)
  3. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana
    Katika nchi ya walio hai
    Umngoje Bwana, uwe hodari,
    Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana. (K)

SOMO 2: Flp. 3: 17- 4:1

Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo, mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani. Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Basi ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.

SHANGILIO Mt. 17:5
Sauti ya Baba ilitoka katika wingu jeupe:
“Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye.”

INJILI: Lk. 9: 28b-36

Yesu aliwatwaa Petro na Yohane na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro akimwambia Yesu, “Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo.” Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona.

TAFAKARI
MUNGU HADANGANYI WATU, TUMSIKILIZE VYEMA: Injili ya leo na masomo mawili yanayoisindikiza inakuja na wazo hili. Mungu ametuahidi uzima wa milele baada ya maisha haya ya taabu. Ametuahidi, tukigaagaa na upwa hatutakula wali mkavu, tukichumia juani tutalia kivulini na kadhalika. Ahadi hizi ametolea ushahidi kwa kumruhusu Yesu, atakayekuwa mjumbe na mwalimu mkuu wa wanadamu, ageuke sura mbele ya mitume wake watatu kwenye mlima Tabori, kwenye nyanda za Galilaya. Kwa nini mitume hao walipata fursa ya kumshuhudia Yesu alipokuwa anageuka sura? Majibu yanaweza kuwa ya namna nyingi lakini tumakinike na jibu lifuatalo. Petro alikuwapo hapo ili kama mkuu wa Kanisa atakaloliacha atoe ushuhuda. Yakobo alikuwapo hapo kwa sababu angelikuwa mtume wa kwanza kuuawa hivyo aisone kama amedanganywa na Yohane alikuwapo hapo kwa vile atakuwa wa mwisho kuteseka kwa ajili ya Yesu asikate tamaa. Mungu hawadanganyi wanadamu. Mmakonde mchonga vinyago hawezi kuzidanganya sanamu zake mwenyewe. Ahadi za Mungu ni thabiti hata kama wanadamu wataona unapita muda mwingi kabla ya utekelezaji wake. Lakini hapo tusisahau kwa Mungu muda una hesabu zingine: miaka elfu moja ni kama siku moja na siku moja kama miaka elfu moja (Zab 90:4).
Somo la kwanza linatusimulia jinsi Mungu alivyowekeana ahadi na Abrahamu kwamba atapata uzao mkubwa wa kumrithi. Tunajua sote kwamba Mungu aliitimiza ahadi hiyo kwa uzao wa Isaka na baadaye Yakobo. Somo la pili linatuletea mawaidha ya Mtume mzoefu, Paulo. Mtume Paulo anasema anajitahidi kuwa mwaminifu katika kauli, maneno na maisha yake kwa ujumla na hivyo angependa watu wengine wajitahidi kumwiga yeye na siyo watu walaghai wanaojisingizia kumtumikia Mungu huku akilenga kuyahudumia matumbo yao tu. Ndipo anasema watu kama hao wanakuwa watu wa ovyo kwa vile wanajitafutia utukufu wao binafsi.
Kwa kujumlisha masomo yanatuambia Mungu pekee yake ndiye mwenye kuweka ahadi za kweli. Tusitilie mashaka ahadi za kimungu maana hadanganyi wala hadanganywi. Wengine wameweka ahadi za upadre, nadhiri za kitawa na viapo. Kwa namna hii, tujikumbushe kila siku kwamba ahadi ni deni na dawa ya deni ni kulipa. Yeye ametuahidia kutupatia uzima wa milele lakini tusipotimiza ahadi zetu atatutupa jehanamu kama alivyoahidi pia. Tusilitafute, tutalipata!

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, utusaidie siku zote kuzikumbuka na kuzitimiza ahadi zetu. Amina.