SOMO I: Kum. 26:16-19
Musa aliwaambia watu: “Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote. Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiza sauti yake; naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa iliyotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote; na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, kama alivyosema.”
Wimbo Wa Katikati: Zab. 119:1-2, 4-5, 7-8
- Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
K. Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
- Wewe umetuamuru mausia yako,
Ili sisi tuyatii sana.
Ningependa njia zangu ziwe thabiti
Nizitii amri zako. (K) - Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.
Nitazitii amri zako, Usiniache kabisa.
INJILI: Mt. 5: 43-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, “Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;” lakini mimi nawaambia, “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”
TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUPENDANA: Ukristo unatudai kupendana daima. Tena unatutaka tusiwe na maadui. Maadui katika maisha hutokana na mtu kuyaweka maslahi yake mbele sana kuliko ya wengine. Hivyo anatengeneza maadui kwa wale anaowaona kuwa kikwazo kwake. Na hapo huanza kuonyesha tabia zinazoashiria uadui. Kristo katika injili anatutaka tuwapende adui zetu na tuwaombee wale wanaotuudhi. Kibinadamu hivi ni vigumu sana. Hebu nitoe mfano, kwaya moja huenda inaichukia kwaya nyingine. Ukijaribu kutafuta sababu ya chuki hii huioni. Unajiuliza wote wanafanya utume mmoja nao ni kumuimbia Bwana. Ukristo unatialika kuleta upatanisho na kuuondoa uhasama. Ka mwanadamu ni vigumu ila kwa Mungu inawezekana kwa sababu jitihada za Mungu ni kuondoa uadui kati ya watu. Na moja ya njia bora za kumaliza uadui ni kumfanya adui kuwa rafiki. Hivyo kwa kumpenda utamuonyesha upendo naye taratibu anaacha ubaya wake ni kuwa mtu mwema. Kwa wanaotuudhi tuwaombee tu ili wabadilike na kuwa wema kwetu.
SALA: Ee Mungu unishushie moto wa mapendo yako niweze kuwapenda hata adui zangu.