Machi 11, 2022; Ijumaa: Juma La 1 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Eze. 18: 21-28

Bwana asema hivi: mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa. Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata moja wapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana Mungu; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi? Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuicha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, na katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. Lakini ninyi mwasema, njia ya Bwana si sawa. Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Israeli; je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, atakufa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 130

 1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia.
  Bwana, uisikie sauti yangu.
  Masikio yako na yasikilize
  Sauti ya dua zangu.

K: Bwana kama Wewe ungehesabu maovu,
Ee Bwana, nani angesimama?

 1. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
  Ee Bwana, nani angesimama?
  Lakini kwako kuna msamaha,
  Ili Wewe uogopwe. (K)
 2. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja
  Na neno lake nimelitumainia.
  Nafsi yangu inamngoja Bwana,
  Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
  Naam, walinzi waingojavyo asubuhi. (K)

INJILI: Mt. 5: 20-26

Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Maana nawaambia ya kwamba, “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, “Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu.” Bali mimi nawaambieni, “Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.” Amin, nakuambia, “Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA UPATANISHO: Maishani, huwa tunawakosea wengine nasi pia hukosewa. Lakini Je, sisi hufanya vipi tunapokosewa? Wengine huweka kinyongo na chuki. Katika Injili Kristo anazungumzia amri ya kuua lakini zaidi anaitaja hasira. Kwa kweli kuua ni matokeo ya hasira. Mpaka mtu afikie hatua ya kuua basi atakuwa ametunza chuki na hasira kwa muda wa kutosha. Kuondokana kabisa na dhambi ya kuua tunapaswa kutoendeleza kisasi, kutolea chuki na kukomaza hasira. Ndiposa tunatakiwa kuwa watu wa kupatana. Kristo hataki tuishi na vinyongo au hasira na wenzetu. Anatutaka tupatane na ndugu zetu kabla ya kujongea madhabahuni kwa sadaka. Na hata kama sisi ndiyo tumekosewa, tusisubiri aliyetukosea aanze kututafuta na kuomba msamaha bali anatutaka tuache sadaka na tukatafute upatanisho kabla ya kuendelea na matoleo. Kwa maneno mengine anatutaka tuwe wa kwanza kushughulikia upatanisho pindi tuonapo kuwa wenzetu wametukosea. Kwaresima ya mwaka huu itujenge na kutufanya kuwa watu wa upatanisho daima.

SALA: Ee Mungu wa rehemu unijalie moyo wa utayari wa kupatana na wengine hata kama wao ndiyo chanzo cha kukosana kwetu.