Machi 10, 2022; Alhamisi: Juma La 1 La Kwaresima

Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Est. 14:1-14

Malkia Esta naye alimkimbilia Bwana, akishikwa na uchungu wa mauti. Akazivua nguo zake za fahari akavaa nguo za huzuni na kilio, na badala ya manukato mazuri alijitia majivu na samadi kichwani; akajinyenyekesha mwili wake, hata mahali pa mapambo ya furaha alijifunika kwa nywele zake zilizofumuliwa. Akamwomba Bwana wa Israeli, akisema, “Bwana wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila Wewe; maana hatari yangu imo mkononi mwangu. Tangu nilipozaliwa katika kabila ya jamaa yangu, nimesikia ya kuwa Wewe, Bwana, ulimchagua Israeli katika mataifa yote, na baba zetu katika jamaa zao, kuwa urithi wa daima, ukawatimilizia yote uliyoyaahidi. Utukumbuke, Ee Bwana; ujifunue wakati wa taabu yetu; unipe moyo thabiti, Ee mfalme wa miungu na Bwana wa milki zote. Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuza moyo wake apate kumchukia yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye. Lakini utuokoe sisi kwa mkono wako; unisaidie mimi niliye peke yangu, bila msaidizi mwingine ila Wewe, Bwana.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 138:1-3, 8-9

 1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
  Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
  Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu
  Nitalishukuru jina lako.

K: Siku ile niliyokuita uliniitikia,
Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.

 1. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
  Kwa maana umeikuza ahadi yako,
  Kuliko jina lako lote.
  Siku ile niliyokuita uliniitikia
  Ukanifariji nafsi yangu kwa kunitia nguvu. (K)
 2. Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
  Bwana atanitimizia mambo yangu;
  Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
  Usiziache kazi za mikono yako. (K)

INJILI: Mt. 7: 7-12

Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA SALA: Jambo lingine muhimu katika kipindi hiki cha Kwaresima ni sala. Sala ni kuongea na Mungu wetu. Kumpelekea maombi, sifa na shukurani zetu. Katika kuomba tunategemea Mwenyezi asikilize na kutujalia tumuombayo. Si ajabu katika maisha kuwa mtu anaweza kuwa ameomba jambo kwa Mungu na kukata tamaa ya kuendelea kuomba baada ya kuona halipati. Katika injili Kristo anasisitiza tuombe na tutapewa, tutafute na tutaona kisha tubishe hodi na tutafunguliwa. Kristo anatuhakikishia kuwa sala zetu Mungu anazisikia na kuzipokea. Mungu ni Baba yetu Mwema. Na daima anatutakia mema wanawe. Kamwe hawezi kupuuza maombi yetu. Kristo anatoa mfano wa baba zetu wa hapa ulimwenguni jinsi wanavyopambana kutupatia yale tuwaombayo. Baba yetu aliye mwema ni zaidi ya baba zetu wa ulimwenguni hivyo yeye yupo tayari kutujalia yote tumuombayo. Shida inaweza kuwa namna Mungu anavyotujalia yale tumuombayo. Yeye hutujalia kwa namna aonavyo yeye kuwa ni bora. Hatuna haja ya kuwa na shaka kuwa atatujalia tumuombalo. Ila sisi kazi yetu iwe kuomba sana, tukiona kimya tutafute kwa nguvu zote na kisha tunabidsha mlango sana tukiamini Mungu atatusikia.

SALA: Ee Mungu usikilize sala zetu. Usikie kuomba kwetu.