Machi 9, 2022; Jumatano: Juma La 1 La Kwaresima

Mt. Fransiska wa Roma, Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Yon. 3: 1-10

Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, “Ondoka uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari nitakayokuamuru.” Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu, Yona akaanza kuuingia mji kwa mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.” Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata yeye aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake, kusema, “Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili tusiangamizwe?” Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:1-2, 10-11, 16-17

 1. Ee Mungu, unirehemu,
  Sawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.

K: Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutaudharau.

 1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
 2. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
  Moyo uliovunjika na kupondeka. (K)

INJILI: Lk. 11: 29-32

Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, “Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.”

TAFAKARI
ISHARA YA YONA: Bado hata katika nyakati hizi watu wanataka ishara. Wanatafuta ishara popote wasikiapo. Wanapenda maigizo na mazingaombwe. Hawataki kusimama katika kweli ya imani. Si ajabu. Hili halikuanza leo. Katika injili tunamuona Kristo akiwashutumu watu wa kizazi chake kuwa walikuwa wakitafuta ishara. Naye anasema ishara pekee watakayopewa ni ishara ya Yona. Ishara ya Yona ni kile kitendo cha kumezwa katika tumbo la nyangumi kwa siku tatu na baadaye kutemwa kwenye nchi kavu. Kristo analifananisha tukio hilo na mateso na kifo chake ambapo baada ya siku tatu naye atafufuka. Ufufuko wa Kristo ndiyo tukio la muujiza mkubwa kabisa kuliko yote. Kwa sasa hatuhitaji muujiza mwingine ili kumwamini Kristo. Ufufuko wake ni uthibitisho tosha kuwa yeye ni mshindi dhidi ya dhambi na mauti. Kwa kufufuka kwake ametia muhuri uhalisia kuwa yeye ni tumaini la maisha baada ya kifo. Kwa kufufuka kwake anatuhakikishia sote kuwa kwa kumfuata yeye nasi tunakuwa na uhakika wa maisha baada ya kifo yaani uzima wa milele. Tuamini juu ya ufufuko wake na kuishi vyema ufuasi wetu.

SALA: Ee Bwana Yesu Kristo unijalie imani hai, nikuamini bila kutafuta ishara.