Machi 7, 2022; Jumatatu: Juma La 1 La Kwaresima

Wat. Perpetua na Felisita, Mashahidi
Kumbukumbu
Urujuani
Zaburi: Juma 4
SOMO 1: Law. 19:1-2, 11-18

Bwana akanena na Musa, akamwambia, “Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli,” uwaambie, “Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu. Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo. Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang’anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi. Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana. Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; Mimi ndimi Bwana. Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake. Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 19:7-9, 14

  1. Sharia ya Bwana ni kamilifu,
    Huiburudisha nafsi.
    Ushuhuda wa Bwana ni amini,
    Humtia mjinga hekima.

K: Bwana unayo maneno ya uzima wa milele.

  1. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
    Huufurahisha moyo.
    Amri ya Bwana ni safi,
    Huyatia macho nuru. (K)
  2. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
    Kinadumu milele.
    Hukumu za Bwana ni kweli,
    Zina haki kabisa. (K)
  3. Maneno ya kinywa change,
    Na mawazo ya moyo wangu,
    Yapate kibali mbele zako, Ee Bwana,
    Mwamba wangu, na mwokozi wangu. (K)

INJILI: Mt. 25:31-46

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Hapo Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama mcungaji abaguavyo kondoo na mbuzi; atawaweka kondoo wake wa kuume, na mbuzi wake wa kushoto.”Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wa kuume, “Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme, mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.”
Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, “Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?” Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, “Kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, “Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe; nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.” Ndipo hao pia watajibu, wakisema, “Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?” Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, “Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.” Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA MATENDO YA HURUMA: Wanadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwanadamu ameinuliwa sana miongoni mwa viumbe wengine. Mwanadamu ni kiumbe cha thamani sana cha Mwenyezi Mungu. Yatupasa kuliona hilo katika wenzetu. Wanadamu yatupasa kuthaminiani sisi kwa sisi. Yatupasa kujaliana. Katika somo la injili Kristo anaweka bayana kuwa siku ya hukumu watu watabaguliwa kutokana na namna walivyowatendea wengine wangali hapa duniani. Watu watabaguliwa kutokana na matendo ya huruma walioonesha kwa wengine. Matendo hayo ni kulisha wenye njaa, kunywesha wenye kiu, kukaribisha wageni, kuvesha walo uchi kutembelea wagonjwa na kutembelea wafungwa. Kristo anapigilia msumari kwa kusema kadiri tunavyowatendea wenzetu tunamtendea yeye mwenyewe. Kipindi hiki cha kwaresima tukutane na Mwenyezi Mungu kupitia wahitaji mbalimbali. Kadiri Mungu alivyotujalia tutende kwa ukarimu. Tufanye matendo ya huruma.

SALA: Ee Mungu uuguse moyo wangu niwe mkarimu kwa wahitaji katika kutenda matendo ya huruma.