Machi 6, 2022; Jumapili: Jumapili Ya 1 Ya Kwaresima

SOMO 1: Kum. 26: 4-10

Musa aliwaambia Waisraeli wote: “Naye kuhani atakipokea kikapu mkononi mwako, akiweke chini mbele ya madhabahu ya Bwana, Mungu wako.” Nawe ujibu, ukaseme mbele za Bwana Mungu wako, “Baba yangu alikuwa Mwarami karibu na kupotea, akashuka Misri akakaa huko ugenini, nao ni wachache hesabu yao; akawa taifa kubwa huko, yenye nguvu na watu wengi. Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu. Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali. Na sasa, tazama, nimeleta malimbuko ya mazao ya ardhi uliyonipa, Ee Bwana.” Kisha ukiweke chini mbele za Bwana, Mungu wako, ukasujudu mbele za Bwana, Mungu wako.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 91:1-2, 10-15

 1. Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
  Atakaa katika uvuli wake mwenyezi,
  Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu.
  Mungu wangu nitakayemtumaini.

(K) Ee Bwana, uwe pamoja nami katika taabu zangu.

 1. Mabaya hayatakupata wewe,
  Wala tauni haitaikaribia hema yako.
  Kwa kuwa atakuagizia malaika wake
  Wakulinde katika njia zako zote. (K)
 2. Mikononi mwako watakuchukua,
  Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.
  Utawakanyaga simba nyoka
  Mwana-simba na nyoka utawaseta kwa miguu. (K)
 3. Kwa kuwa amekaza kunipenda
  Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
  Kwa kuwa amenijua jina langu.
  Ataniita nami nitamwitikia;
  Nitakuwa pamoja nae taabuni,
  Nitamwokoa na kumtukuza. (K)

SOMO 2: Rum. 10: 8-13

Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo. Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao; kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.

SHANGILIO: Mt. 4 :4
Mtu hataishi kwa mkate tu,
Ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu

INJILI: Lk. 4: 1-13

Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka Yordani, akaongozwa na Roho muda wa siku arubaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Na siku hizo alikuwa hali kitu; hata zilipotimia, aliona njaa. Ibilisi akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu.” Akampandisha juu, akamwonyesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja. Ibilisi akamwambia, “Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa yeyote kama nipendavyo. Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako.” Yesu akajibu akamwambia, “Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” Akamwongoza mpaka Yerusalemu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, ‘Atakuagizia malaika zake wakulinde;’ na ya kwamba, ‘Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.”’ Yesu akajibu akamwambia, “Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.” Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.

TAFAKARI
TUVIWAHI VISHAWISHI KABLA HAVIJAWA DHAMBI: Wazo hili linatoka katika Injili tuliyosoma na linaungwa mkono na masomo mawili yanayoisindikiza. Kwa taarifa yetu, kuna vyanzo vinne vya vishawishi: mtu mwenyewe, mazingira, Shetani na wengine. Mtu kwa tamaa na mawazo yake anaweza kujitumbukiza katika vishawishi mbalimbali (Yak 1;12-15). Mazingira yanaweza kuwa mabaya hata kumzalia mtu vishawishi. Shetani ni mwovu anayetamani wanadamu wafarakane na Mungu na hivyo watumbukie pamoja naye katika moto alioandaliwa kwa ajili yake na wafuasi wake. Hatimaye, wengine, kwa mawazo, maneno na matendo yao wanaweza kumshawishi mtu hata akaishia pabaya. Katika Injili ya leo, tunaweza kuzingatia chanzo cha kwanza na cha tatu. Ndio maana mtu akisema vishawishi anavyokabiliana navyo Yesu vinaweza kusababishwa na mawazo yake mwenyewe kama mwanadamu (Yak 1:12-15) atakuwa hajakufuru. Vile vile mtu mwingine akisema chanzo cha vishawishi hivyo kilikuwa Ibilisi hatakuwa amekosea. Tangu mwanzo, nia ya Shetani ilikuwa kumsepetua Yesu akwame katika mradi wa kuwakomboa wanadamu. Hapa tunaweza kujadiliana sana.
Jambo la maana kwetu ni kujifunza kutoka kwa Yesu jinsi alivyovikabili vishawishi visigeuke dhambi. Aliviwahi mapema kabisa. Injili inamwonesha Shetani akijaribu kumnasa Yesu kwa kunukuu Maandiko Matakatifu na laghai za aina yake. Yesu anaziponda nukuu za Shetani kwa nukuu sehemu bora zaidi. Na mintarafu laghai, Yesu anazing’amua na kumwonesha jinsi shetani anavyoogopa. Mtindo huu wa kumshinda shetani ndiyo ungalikuwa bora kwetu wakati tunapambana na vishawishi. Yafaa tuyajue Maandiko Matakatifu kumshinda Shetani na tujizoeshe kung’amua laghai za Shetani. Uwezo huu anao kila mmoja. Shida yetu ni kwamba tunajidharau hata kujiona hatuna nguvu mbele ya vishawishi. Mungu haruhusu vishawishi vinavyotuzidi au ambavyo hatuoneshi mlango wa kutokea (1Kor 10:11-12).
Pamoja na ukweli kwamba Mungu mwema haruhusu wanadamu tujaribiwe zaidi ya uwezo wetu, tusibweteke. Badala yake tusipojiboresha katika mbinu alizotumia Yesu kuvishinda vishawishi vilivyomfika, tutajinasa wenyewe. Tamaa zetu zinapotuandama kama chanzo cha vishawishi na ikiwa ni Shetani anayetukabili basi atatunasa kirahiai kama wajinga vipofu. Ubaya ni kwamba vishawishi vikichukua mimba huzaa dhambi na dhambi zikikomaa huzaa mauti (Yak 1;12-15). Kumbe heri kuvishinda vishawishi kabla havijageuka dhambi.
Somo la kwanza linaonesha jinsi Mungu alivyowaweka Wayahudi mahali salama baada ya kumlilia na yeye kuona shida yao. Kwa kuonesha kazi hiyo ya Mungu, somo linalenga katika kutuomba wanadamu “tutulizane” na Mungu; tusiwe wazembe tukaenda kujitosa katika mambo yanayosimama kinyume na wema na kazi njema ya Mungu. Aliye mikononi mwa Mungu yu salama sana. Somo la pili linaunga mkono ukweli kwamba mahali pa salama pa mwanadamu kusudi awe na nguvu ya kukabiliana na ya ulimwengu huu ni kubaki na Mungu. Kifupi, vishawishi vinaweza kukabilika ikiwa mmoja amejibanza kwa Mungu.

SALA: Ee Bwana Yesu, uliviwahi vishawishi kabla havijageuka dhambi. Tudumishe katika mbinu zako kusudi nasi tusishindwe na vishawishi. Amina.