Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Isa. 58: 9b-14
Bwana asema hivi: kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usiihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe; wala kuyatafuta ya kupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.
Wimbo Wa Katikati: Zab. 86:1-2, 3-4,5-6
- Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
Maana mimi ni maskini na mhitaji,
Unihifadhi nafsi yangu,
Maana mimi ni mcha Mungu.
Wewe uliye Mungu wangu,
Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
K: Ee Bwana, unifundishe njia yako;
Nitakwenda katika kweli yako.
- Wewe, Bwana unifadhili,
Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
Maana nafsi yangu yakuinulia Wewe Bwana. (K) - Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
Umekuwa tayari kusamehe,
Na mwingi wa fadhili,
Kwa watu wote wakuitao.
Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)
INJILI: Lk. 5: 27-32
Siku ile: Yesu aliona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, “Nifuate.” Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?” Yesu akajibu akawaambia, “Wenye afya hawana haja ya tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.”
TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA TOBA: Ni ukweli usiopingika. Kama huugui unaweza usijue mengi kuhusu huduma ya afya. Kama huna matatizo ya moyo huwezi kujua maendeleo ya tiba yaliyopo hapa nchini na shughuli zinazoendelea katika taasisi ya mgonjwa za moyo. Kama hujapata tatizo la mifupa au mishipa huwezi kuona umuhimu wa taasisi ya matatizo haya. Kama hujaugua kisukari huwezi kukutana na madaktari bingwa wa ugonjwa huo. Ukipata tezidume utaambiwa tu hospitali gani ina madaktari bobezi wa shida hiyo. Pia ukipata tatizo la figo ndo utajua hospitali ngapi zinaweza kutoa huduma ya kusafisha damu katika eneo ulilopo. Usipougua hata majina ya vipimo vitakuwa vya ajabu kwako. Kama Echo, CT scan na MRI vitakuwa vya ajabu. Hakika usipougua hutahitaji tabibu. Unapojiona wewe ni mtu mwema hukufanya usihangaikie wokovu wako. Kwanza tukubali kuwa kama wanadamu sisi sote tunahitaji wokovu. Na wokovu unapatikana katika kumuamini Kristo. Kristo amekuja kutuita ili sisi wadhambi tupate kutubu. Tuchunguze vyema dhamiri zetu na tuchangamkie toba hasa katika kipindi hiki cha kwaresima. Kwaresima hii itufanye tuwe watu wa toba.
SALA: Ee Mungu uuchunguze moyo wangu. Unijalie moyo wa toba.