Machi 4, 2022; Ijumaa: Ijumaa Baada Ya Majivu

Mt. Kasimiri
Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Isa. 58: 1-9

Bwana Mungu asema hivi: “Piga kelele, usiache, paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, ‘Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii?”’ Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, nakupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Si siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana. Je! saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Sio kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na bwana ataitika; utalia, naye atasema, “Mimi hapa.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:3-6a, 18-19

 1. Maana nimejua mimi makosa yangu,
  Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
  Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
  Na kufanya maovu mbele za macho yako.

K: Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutadharau.

 1. Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
  Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
  Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni
  Nawe wanijulisha hekima kwa siri. (K)
 2. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
  Uzijenge kuta za Yerusalemu .
  Ndipo utakapopendezwa na dhabihu ya haki;
  Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K)

INJILI: Mt. 9: 14-15

Siku ile: Yesu alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, “Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawaambia, “Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA FUNGA YA KIROHO: Kati ya mazoezi ya kiroho muhimu kufanyika katika kipindi hiki cha kwaresima ni kufunga. Mafarisayo walilichukulia tukio la kufunga kama sehemu ya kutafuta sifa kwa watu. Hata wanafunzi wa Yohane katika Injili tunaambiwa kuwa walikuwa wakifunga ndio maana wakashangaa kwa nini wanafunzi wa Kristo hawafungi. Jibu la Kristo ni kuwa muda wa kufunga utafika nao watatakiwa kufunga. Tunapofunga tunajikatalia kula na kunywa. Tukio hili la kiroho hutubandua katika vionjo na mahitaji ya mwili na kuipa roho fursa ya kujiunganisha na muumba wake. Kristo mwenyewe alifunga mara kadhaa. Kabla ya kuanza utume wake alifunga kwa siku arobaini mpaka akaona njaa. Alifunga kwa ajili ya kukusanya nguvu kabla ya kuanza utume wake duniani. Kufunga kuna faida nyingi za kiroho na kimwili lakini Zaidi, ni tendo la ibada linalotupa nguvu za kiroho katika vita vyetu hapa duniani. Hivyo kufunga kwetu kuambatane na matendo mema ili Mungu apokee swahumu yetu asije akaikataa kama tusomavyo katika somo la kwanza. Kufunga kwetu kuwe kwa kiroho na kutupe matunda ya kiroho.

SALA: Ee Mungu uipokee funga yangu na sala zangu nikutoleazo wakati huu wa kwaresima.