Machi 3, 2022; Alhamisi: Alhamisi Baada Ya Majivu

Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Kum 30: 15-20

Musa aliwaambia watu akisema: “Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia, hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. Nazishuhudisha mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kupenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.”

Wimbo Wa Katikati: Zab. 1:1-4,6

 1. Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki;
  Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
  Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
  Basi sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
  Na sheria yake huitafakari mchana na usiku
  K: Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake.
 2. Naye atakuwa kama mti uliopandwa
  Kandokando ya vijito vya maji,
  Uzaao matunda yake kwa majira yake,
  Wala jani lake halinyauki;
  Na kila alitendalo litafanikiwa. (K)
 3. Sivyo walivyo wasio haki;
  Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
  Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
  Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)

INJILI: Lk. 9: 22-25
Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?”

TAFAKARI
KWARESIMA NI KIPINDI CHA KUJITOA: Kwaresima imefika. Ni kipindi kingine tena cha kuangalia maisha yetu na matendo yetu yatusogeze karibu na Mwenyezi Mungu. Injili ya leo yatuhimiza mambo matatu muhimu kwa ufuasi wetu na hasa wakati huu wa Kwaresima. Kwanza kujikana mwenyewe. Maana yake kutumika ipasavyo bila kujali maslahi yetu. Pili ni kujitwika msalaba. Ufuasi si lelemama. Una changamoto zake nyingi tu. Yatupasa kufahamu hilo, kuzikabili changamoto hizo bila kuyumba na kuendelea mbele. Kuvumilia magumu yote ya ufuasi na bado kuendelea kusimama imara katika imani. Changamoto tunazokutana nazo katika ufuasi zina lengo la kutukomaza kiimani. Kukabiliana nazo ndiyo kujitwika msalaba kila siku. Mwisho ni kumfuata Kristo. Kama kweli sisi ni wafuasi wa Kristo basi hatuna budi ila kumfuata Kristo. Kusikiliza anachotuelekeza. Kufuata maongozi yake. Kuachana na yote anayotukataza na hivyo kumuhakisi yeye katika maneno na matendo yetu ili kwa namna tunavyotenda na kusema watu waweze kumuona Kristo kwa kupitia sisi. Kipindi hiki cha kwaresima ni kipindi kizuri kufanya mazoezi ya kujitoa kweli kwa Kristo.

SALA: Ee Mungu, unijalie moyo thabiti wa kujitoa katika ufuasi wangu kwa Kristo.