Machi 02, 2022; Jumatano ya Majivu: Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima (Mfungo Mtakatifu). Matayarisho kwa siku Tatu Kuu za Pasaka. Ni siku ya mafungo (walio kati ya umri wa miaka 18-59; msile nyama (miaka 14 kwenda juu).

Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Yoe. 2:12-18
Lakini hata sasa, asema Bwana, “Nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hugairi mabaya. N’nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa Bwana, Mungu wenu? Pigeni tarumbeta katika Sayuni, takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu; kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, na hao wanyonyao maziwa; bwana harusi na atoke chumbani mwake, na bibi arusi katika hema yake.” Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie kati ya patakatifu na madhabahu, na waseme, “Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, wala usiutoe urithi wako upate aibu, hata mataifa watawale juu yao; kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?” Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.

Wimbo Wa Katikati: Zab. 51:1-4, 10-12, 15

 1. Ee Mungu, unirehemu,
  Sawasawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.
  Unioshe kabisa na uovu wangu,
  Unitakase dhambi zangu.

K: Uturehemu, ee Bwana,
kwa kuwa tumetenda dhambi.

 1. Maana nimejua mimi makosa yangu,
  Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
  Nimekutenda dhambi wewe peke yako,
  Na kufanya maovu mbele za macho yako. (K)
 2. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
 3. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
  Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
  Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
  Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)

SOMO 2: 2 Kor. 5:20-6:2
Ndugu zangu, basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vyinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye. Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, “Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nilikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndio sasa.”

SHANGILIO: Zab. 95:8

Msifanye migumu mioyo yenu;
msikieni sauti ya Bwana.

INJILI: Mt. 6:1-6, 16-18
Siku zile, Yesu aliwaambia wafuasi wake: “Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu.” Amin, nawaambieni, “Wamekwisha kupata thawabu yao.” Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, “Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga,” Amin, nawaambia, “Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”

TAFAAKARI
TUFUNGE TUJIPATANISHE NA MUNGU NA SIYO KWA KUJIONESHA: Ujumbe huu ni jumla ya mawaidha ya Injili na masomo mawili tuliyoyasikia hivi punde. Kwa zoezi la kufunga, Wayahudi walimaanisha kujinyima chakula na maji kwa muda mrefu au mfupi kwa ajili ya kujinyima au kujinyenyekesha. Jina la lingine la mfungo lilikuwa “kuitesa roho.” Kabla ya kupelekwa uhamishoni Babiloni (mwaka 587 K.K.), Wayahudi walikuwa na siku moja tu ya kufunga, ile siku ya toba ya kitaifa (“Yom Kippur” – Law 16:29. 31; Hes 29:7, Yer 36:6). Lakini pamoja na siku hiyo maalumu ya kufunga, watu waliweza kufunga kwa sababu mbili: kukiri kuvunja amri za Mungu na kujiepusha na adhabu ya Mungu (1Fal 21:9-12). Baada ya kurudi uhamishoni Babiloni zikaongezeka siku nne zingine za kufunga: (tarehe 17 Tammuz) kuomboleza kuvunjwa kwa kuta za Yerusalemu, (tarehe 9 Ab) kuomboleza kubombolewa kwa hekalu, tarehe 3 Tishri kukumbuka mfungo wa Gedaliya na tarehe 10 Tebeth kukumbuka kuanza kuzingirwa mji wa Yerusalemu. Kwa upande wao Mafarisayo wakajiongezea mbili zingine: Jumatatu na Alhamisi, wakisema, “Mungu alikwenda kuonana na Mungu na kupewa mbao za amri kumi Jumatatu na akarudi Alhamisi (Lk 18:12).”
Malengo ya kufunga yalibaki bado mawili: kuombolezea dhambi kupoza ghadhabu ya Mungu na kuombolezea dhambi ili kupata rehema. Hata hivyo, kufunga kwenyewe kulifanywa kwa mbwembwe na kujionesha kwingi. Walijitia majivu, walirarua nguo zao, walivaa magunia na kadhalika kwa nia ya kuonekana na watu kwamba walikuwa wacha Mungu na watu wa ibada. Watu walikunja nyuso zao na kuwataka wengine wafyate mikia kwa sababu wao walikuwa katika kufunga. Ndiyo kasoro hizi Yesu anazozizungumzia katika Injili ya leo. Wakati wa Kwaresima tunatakiwa kufanya mazoezi ya kufunga, kusali na kuwasaidia maskini na wahitaji lakini si kwa mbwembwe na kujionesha kama Wayahudi. Matendo hayo yanatakiwa yatendwe kwa toba ya kujipatanisha na Mungu. Mwanadamu anatakiwa afunge, asali na kuwasaidia wahitaji kwa ajili ya Mungu na siyo kwa ajili ya binadamu.
Kuendana na uelewa huu somo la kwanza limekaa vizuri sana. Linasisitiza watu kufunga kwa kusudi la kumrudia Mungu. Wanaombwa wararue mioyo yao na wala si mavazi yao kusudi Bwana awaonee huruma na kughairi ghadhabu yake. Somo la pili linaweka bayana dhana ya upatanisho. Linawataka wanadamu kukazia upatanisho na Mungu kwa sababu mradi mkubwa wa Mungu, mradi uliomleta Mwanaye ulimwenguni ni upatanisho. Kama ndivyo wajibu upatanishi aliouanzisha Mungu kwa wao kujipatanisha na Mungu. Pungufu ya hapo itakuwa kufuja matashi mema ya Mungu.
Majivu tunayopakwa usoni ni majivu ya matawi tuliyotumia wenyewe kumshangilia Yesu Kristo mwaka jana kwenye Sikukuu ya Matawi. Yanatumika majivu ya namna hiyo sio kwa ajili ya kutukumbusha sisi tuliotoka vumbini kwamba siku moja tutarudi tulikotoka. Pia ni ya kutukumbusha kwamba sisi tu vinyonga wakubwa, watu wepesi kugeuka kwa mawazo na matendo.
Tukijumlisha yote tuliyosema turudie kauli yetu: tufunge tujipatanishe na Mungu na siyo kwa kujionesha kwa wanadamu. Wanadamu huishia kustaajabu lakini Mungu huishia kusamehe, kurehemu na kutuza uzima wa milele.

SALA: Ee, Mungu, tusaidie tuwe na Kwaresima yenye manufaa makubwa ya kiroho. Tusali, tufunge na tuwasaidie wenye dhiki kwa ajili yako na si kwa ajili ya sisi kujionesha kwa wenzetu. Amina.