Machi 1, 2022; Jumanne: Juma La 8 La Mwaka 2

Kijani
Zaburi: Juma 4
SOMO I: 1Pet. 1:10-16

Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia. Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza, za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, ‘Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.’

Wimbo Wa Katikati: Zab. 98: 1-4

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
  Mkono wa kuume wake mwenyewe,
  Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
  (K) Bwana ameufunua wokovu wake.
 2. Bwana ameufunua wokovu wake,
  Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
  Amezikumbuka rehema zake,
  Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
 3. Miisho yote ya dunia imeuona
  Wokovu wa Mungu wetu.
  Mshangilieni Bwana, nchi yote,
  Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

INJILI: Mk. 10:28-31
Petro alimwambia Yesu, “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.” Yesu akasema, “Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza.”

TAFAKARI
ANAYEJITOA KWA MUNGU HAPOTEZI KITU: Wito unahitaji watu kuitikia utume mbalimbali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Sio wote wanaoitwa wanaitikia mwaliko huu. Wengine hukataa. Na wanaweza kuwa na sababu nyingi za kukataa wito huo. Sababu kubwa yaweza kuwa wito unaingilia mipango ya mtu. Mtu atatakiwa kuacha familia, ndugu, mali na hata kuwa mbali na nyumbani. Mtu anaweza kuhesabu hivi kama hasara ya kuitikia wito. Swali ya Mtume Petro katika Injili laweza kuwa swali la wengi wetu. Tumeacha vyote, tutapata nini? Kristo anatutoa hofu kwa kujitoa kwetu na anapotuhakikishia kuwa anayejitoa kwa ajili yake atapewa mara mia na zaidi uzima wa milele. Tunataka nini tena? Kikubwa Kristo anatuhakikishia kuwa anayejitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu hapotezi kitu. Hivyo basi, tutoe ushauri kwa yeyote anayeisikia sauti ya Mungu lakini amekuwa akisitasita kuitika wito huu. Labda anakataa kwa sababu ya mali, lakini vitu vyote ni vya Mungu. Tukubali atutumie sisi kama vyombo vyake viteule.

SALA: Ee Bwana unijalie moyo wa utume, nijitoe kwako bila kuangalia maslahi binafsi.