Februari 28, 2022; Jumatatu: Juma La 8 La Mwaka

SOMO 1: 1Pet. 1: 3-9
Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kriso, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho. Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali; ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo. Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu.
Wimbo Wa Katikati Zab. 111: 1-2,5-6,9-10

  1. Aleluya,
    Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
    Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
    Matendo ya Bwana ni makuu,
    Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
    (K) Atalikumbuka agano lake milele.
  2. Amewapa wamchao chakula;
    Atalikumbuka agano lake milele.
    Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
    Kwa kuwapa urithi wa mataifa. (K)
  3. Amewapelekea watu wake ukombozi.
    Ameamuru agano lake liwe la milele,
    Jina lake ni takatifu la kuogopwa. (K)
  4. Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima,
    Wote wafanyayo hayo wana akili njema,
    Sifa zake zakaa milele. (K)

INJILI: Mk. 10:17-27

Yesu alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, “Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?” Yesu akamwambia, “Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako.” Akamwambia, “Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu.” Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, “Umepungukiwa na neno moja, Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote. Uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.
Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, “Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu!” Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, “Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Nao wakashangaa mno, wakimwambia, “Ni nani, basi, awezaye kuokoka?” Yesu akawakazia macho, akasema, “Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu.”

MAISHA YA MBINGUNI NI YA RAHA TU: Mhusika anayeelezwa katika injili tunaambiwa alimwendea Yesu mbio. Hili ni ashirio kuwa ana hamu ya kujua kitu fulani ambacho huenda kimemsumbua kwa muda mrefu na hivi alitaka apate jibu toka kwa Yesu. Swali lake, “Mwalimu mwema nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele?” Yesu anamjibu kwa kuchambua nae kundi la pili la Amri za Mungu, ambalo linazungumzia mahusiano kati ya mwandamu na mwanadamu (amri ya 4 hadi 10) Kikwazo kinachoonekana kwa huyu ni kukosa ukarimu, kuwa na ubinafsi, kung’ang’ania mali. Twaweza kuwa watu wazuri sana wa kufuata amri/sheria/taratibu lakini shida tunakosa matendo ya huruma, ukarimu na utu. Kanisani twaenda sana, ila shida za wengine hatuzitatui japo uwezo tunao. Leo hii Kristo anatukumbusha kuwa pamoja na kufuata sheria au taratibu, basi tukamilishe hayo kwa kushirikishana tuliyojaliwa na Mungu.