Februari 26,2022; Jumamosi: Juma La 7 La Mwaka

SOMO 1: Yak.5: 13-20
Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinye; na mvua haikunya juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.
Ndugu zangu, ikiwa mtu wa kwenu amepotelea mbali na kweli, na mtu mwingine akamrejeza; jueni ya kuwa yeye amrejeshaye mwenye dhambi hata atoke katika njia ya upotevu, ataokoa roho na mauti, na kufunika wingi wa dhambi.

Wimbo Wa Katikati Zab. 141: 1-3, 8

 1. Ee Bwana, nimekuita, unijie hima,
  Uisikie sauti yangu nikuitapo.
  Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba
  Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.
  (K) Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba.
 2. Ee Bwana, uweke mlinzi kinywani pangu,
  Mngojeze mlangoni pa midomo yangu.
  Macho yangu yanakuelekea Wewe, Mungu Bwana,
  Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. (K)

INJILI: Mk .10: 13-16
Makutano walimletea Yesu watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, “Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa.” Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabariki.

TAFAKARI
SAKRAMENTI NI DARAJA LA KUENDEA WOKOVU: Kristo alitupatia Sakramenti saba katika Kanisa Katoliki ili zitufae kwa wokovu wetu. Hizi ni ishara wazi inayooneka inayobeba neema ya Mungu isiyoonekana. Mpako Mtakatifu ni mojawapo wa Sakramenti hizi. Sakramenti hii huweza kupewa; wagonjwa, wazee, walio kufani, wanaosafiri na hivi kuwa na wasiwasi mfano safari za mbali kama kupanda ndege, wanaotegemea kujifungua au kufanyiwa upasuaji. Hii ndio Yakobo anaizungumzia, “Mtu wa kwenu amekuwa hawezi na awaite wazee wa Kanisa wamwombee na kumpaka mafuta”. Wengi wetu tunaogopa Sakramenti hii, tukidhani kuwa eti mtu akipewa mpako Mtakatifu maana yake anakufa, utaona mpaka padre aitwe ili ampe mgonjwa mpako mtakatifu ni baada ya kufikia hatua ya kushindwa kupumua. Kufanya hivi ni kosa, tena ili iwe ya manufaa mazuri, ni vizuri mhusika akaomba mwenyewe, sio wengine kumwombea. Huenda wakati mwingine sisi wa pembeni tunamlazimisha. Tunaalikwa tuukumbatie ufalme wa mbinguni kama watoto. Injili yatuasa hilo na hii ni katika kupokea vyema sakramenti za Kanisa.

SALA: Bwana Yesu tunaomba utujalie tupokee vyema katika hali ya usafi sakramenti zako.