SOMO 1: Yak. 5: 9-12
Ndugu, msinung’unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.
Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.
Wimbo Wa Katikati Zab.103: 1-4, 8-9, 11-12
- Ee nafsi yangu, umhimidi bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema. - Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K) - Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta sikuzote,
Wala hatashika hasira yake milele. (K) - Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)
INJILI: Mk. 10:1-12
Yesu alifika mipakani mwa Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, “Je! ni halali mtu kumwacha mkewe?” Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, “Musa aliwaamuru nini?” Wakasema, “Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha.”
Yesu akawaambia, “Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja, hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, “Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.”
TAFAKARI
UBISHI NI DALILI YA KUTOJIKUBALI: Kila mara tunaalikwa tuwe watu wa kujikubali na kujitambua. Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Mtume Yakobo anatuonyesha umuhimu wa kujitambua. Mwanadamu mara nyingi anajikuta anaapa ili kudhihirishia wengine kuwa si yeye, kwa mfano, jambo limetendeka na hivi wako watakaohisiwa, kila atakayeulizwa atajitetea kwa kuapa na hata kumtaja Mungu, utasikia. “Naapa kwa jina la Yesu sio mimi.” Na kumbe ndiye. Tunapenda kuuridhisha uma kuwa tuko safi. Tunaambiwa ndiyo yetu na iwe ndio na siyo iwe siyo. Swali la Mafarisayo kwa Yesu ni ishara wazi ya kutojikubali na kuwa tayari kubadilika, ndio maana Yesu anawaambia, “Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu”. Mtu wa namna hii ni vigumu kukubali ukweli, ni vigumu kumsahihisha, anakuwa na msimamo usiosaidia.
SALA: Twakuomba Mama Bikira Maria utuombee tuweze kujikubali.